Wednesday, May 11, 2016

WANAFUNZI SHULE YA MSINGI NGAPA TUNDURU WAKOSA MAHALI PA KUSOMEA TANGU MWAKA 2014

Jengo la shule ya msingi Ngapa wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, ambalo limeezuliwa kwa mvua iliyoambatana na upepo mkali mwaka 2014.
Na Steven Augustino,
Tunduru.

WANAFUNZI 589 wanaosoma shule ya msingi Ngapa, wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma wapo katika hatari ya kufanya vibaya katika masomo yao, kutokana na shule hiyo kubomoka na kukosa mahali pa kusomea masomo yao.

Hali hiyo inawafanya wanafunzi hao, kusoma kwa kupeana zamu katika madarasa matatu kati ya saba yanayohitajika wakati wanapokuwa katika vipindi vyao vya masomo darasani.
Jengo ambalo limeezekwa kwa nyasi wanalotumia sasa kusomea.

Tatizo hilo limedumu kwa muda mrefu na kusababisha madarasa manne yaliyopo katika shule hiyo kubomolewa na mvua ya mawe, ambayo iliambatana na upepo mkali Februari 5 mwaka 2014.

Aidha taarifa za awali zinaeleza kuwa, sambamba na kubomolewa kwa madarasa hayo shule hiyo haina hata vyoo vya kujisaidia wanafunzi hao jambo ambalo linawafanya wajisaidie porini kipindi chote tangu mwaka huo, shule hiyo ilipokumbwa na mkasa huo.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti wazazi na walezi wa watoto hao walisema kuwa, kinacho washangaza ni kwamba tangu wakati huo hawajawahi kuwaona viongozi ngazi ya serikali, kwenda kutoa msaada waina yoyote au kufanya jitihada juu ya ujenzi wa vyoo na madarasa hayo yaliyobomoka.

Wananchi hao waliiomba serikali, kupitia Wizara ya elimu kuingilia kati na kuhakikisha shule hiyo inajengwa ili kuwawezesha watoto hao kusoma katika mazingira mazuri.

Katika tukio hilo walisema, pia mvua hiyo ilibomoa nyumba 36 za wananchi waishio karibu na shule ya msingi Ngaga na kuwaacha wakazi wake, wakiwa hawana mahali pa kuishi.

Mwalimu Mkuu  shule hiyo, Christopher Mnipa alithibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kueleza kwamba kuna kila sababu kwa serikali kuchukua hatua za haraka ili kuweza kunusuru hali hiyo.

Tina Sekambo ambaye ni Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Tunduru pamoja na kukiri kuwepo kwa tatizo hilo, alisema kwamba kilichowafanya washindwe kutekeleza ujenzi wa madarasa hayo kinatokana na wananchi kukataa kujitolea kuchangia nguvu zao ili ujenzi uweze kuanza mara moja.

Hata hivyo, alisema Halmashauri hiyo kwa kushirikisha wataalamu wake wanajipanga kwenda kutoa elimu na hamasa kwa wananchi hao kujitokeza kuchangia nguvu zao na halmashauri, iweze kununua vifaa vya ujenzi ili kuweza kumaliza tatizo hilo ambalo limedumu kwa muda mrefu sasa.

No comments: