Monday, May 30, 2016

WAKULIMA WAIOMBA HALMASHAURI KUKAMILISHA UJENZI WA MRADI WA UMWAGILIAJI

Betramu Sanga ambaye ni afisa kilimo (katikati) akiwapa maelekezo juu ya kilimo bora cha zao la mpunga wakulima wa kijiji cha Mabuni kata ya Litumbandyosi wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma.



Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WAKULIMA wanaozalisha zao la mpunga katika mradi wa umwagiliaji Sanga mabuni uliopo kijiji cha Mabuni kata ya Litumbandyosi wilaya ya Mbinga mkoa wa Ruvuma, wameiomba Halmashauri ya wilaya hiyo kufanya jitihada ya kukamilisha ujenzi wa mfereji wa kuleta maji shambani ili waweze kuzalisha zao hilo kwa wingi.

Aidha wameeleza kuwa mfereji huo unaoleta maji shambani ambao una urefu wa mita 5,850 kutoka kwenye banio kuu la umwagiliaji, ambapo zilizojengwa mpaka sasa ni mita 3,175 na kwamba zilizobakia ni mita 2,625 ambazo bado ujenzi wake haujakamilika na kuweza kuleta maji kwenye mashamba yaliyopandwa zao hilo.

Silvester Ngonyani ambaye ni Mwenyekiti wa mradi huo, alisema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ambao walitembelea kwa lengo la kujionea mafanikio wanayoyapata na changamoto mbalimbali ambazo hukabiliana nazo wakulima hao. 


“Hivi sasa kama mfereji huu ungekamilika ujenzi wake malengo yetu ni kuzalisha zaidi ya gunia 40 za mpunga, lakini tunashindwa kufikia lengo hili kutokana na mfereji huu kutokamilika ujenzi na kuweza kuleta maji mengi shambani”, alisema Ngonyani.

Ngonyani alifafanua kuwa wanaiomba pia serikali iwatazame kwa jicho la huruma wakulima wanaozalisha zao la mpunga kwa kuwapatia ruzuku ya pembejeo za kilimo ili waweze kuzalisha mpunga kwa wingi na kuweza kuondokana na umaskini miongoni mwao.

Alisema kuwa mradi wa umwagiliaji Sanga mabuni umesajiliwa kisheria na kwamba ulianza kazi rasmi ya umwagiliaji mwaka 2004, hivi sasa una wanachama 122 wakiwemo wanawake 61 na wanaume 61 ambao hufanya kazi ya kuzalisha zao la mpunga kwa njia ya umwagiliaji.

Theresia Kinyeru ambaye naye ni mkulima na mwanachama katika mradi huo, alitoa ushauri wake akisema kwamba ili waweze kuondokana na kero hiyo ya upatikanaji wa maji, ni vyema serikali ikaweka mpango wa kuwajengea bwawa kubwa la kuhifadhia maji ambalo katika kipindi cha mwaka mzima wataweza maji hayo kuyatumia katika shughuli za umwagiliaji.

Kinyeru alisema kuwa licha ya kuwepo kwa changamoto hizo, lakini wanaushukuru uongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga kwa kuwajengea mradi huo ambao umekuwa ni msaada mkubwa kwao, wameweza kuwa na kipato kwa kujenga nyumba za kisasa ambazo zimeezekwa bati.

No comments: