Wednesday, June 1, 2016

MBUNGE WA MBINGA MJINI SIXTUS MAPUNDA ATOA MSAADA WA JEZI KWA TIMU YA KOMBAINI MBINGA


Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, Oscar Yapesa akipokea vifaa vya michezo kutoka kwa Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Mbinga mjini, Geddy Ndimbo vilivyotolewa na Mbunge wa jimbo hilo Sixtus Mapunda kwa ajili ya timu ya Kombaini ya vijana wa shule za sekondari za halmashauri ya mji huo, ambao itashiriki mashindano ya UMISETA ngazi ya wilaya na mkoa ambayo yanatarajia kufanyika kesho, Juni 2 Mwaka huu.
Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

HALMASHAURI ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, imepokea vifaa vya michezo mpira wa miguu na pete kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Mbinga mjini, Sixtus Mapunda ili viweze kusaidia vijana wanaotoka katika baadhi ya shule za sekondari zilizopo katika mji huo, kushiriki kikamilifu mashindano ya Umoja wa Michezo Sekondari Tanzania (UMISETA) ngazi ya wilaya na mkoa.

Akikabidhi vifaa hivyo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa mji huo, Oscar Yapesa ambavyo ni jezi zenye thamani ya shilingi 650,000 kwa niaba ya Mbunge huyo, Geddy Ndimbo ambaye ni katibu wake alisema kuwa wawakilishi wa timu ya Kombaini ya vijana wa shule hizo, ndio watakaoshiriki mashindano hayo ambayo yanatarajia kuanza kutimua vumbi Juni 2 Mwaka huu katika uwanja wa michezo wa shule ya sekondari Makita uliopo mjini hapa.  
 
Geddy alifafanua kuwa ufadhili huo uliotolewa na Mbunge Mapunda ni endelevu na kwamba lengo ni kutafuta vijana watakaoweza kuunda timu ya mkoa huo, ambao baadaye wataungana na wenzao wa kutoka katika maeneo mbalimbali ndani ya mkoa.

“Idara ya Ofisa utamaduni na michezo pia na elimu ya sekondari tunaipongeza kwa maandalizi inayoyafanya katika kushiriki kikamilifu kwenye mashindano haya, ambayo yataweza kukuza na kuendeleza vipaji kwa vijana wetu”, alisema Geddy.


Alisema kuwa timu hiyo ya Kombaini ya kutoka hapa Mbinga, anapenda kuona inaendelea kufanya vizuri hadi ngazi ya mkoa ili pia iweze kusonga mbele zaidi.

Katibu huyo wa Mbunge wa Jimbo la Mbinga mjini aliongeza kuwa mpango alionao Mbunge Mapunda kwa siku za usoni, anahitaji kuwekeza katika sekta ya michezo kwa vijana wa shule zote za sekondari zilizopo katika jimbo hilo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji huo, Yapesa alishukuru msaada huo uliotolewa na Mbunge huyo ambao unalenga kuwasaidia vijana hao, waweze kufanya vizuri katika sekta ya michezo na kukuza vipaji vyao.

No comments: