Thursday, June 16, 2016

WAVUVI NYASA WALIA NA HALMASHAURI KUPANDISHA BEI YA LESENI ZA UVUVI



Na Mwandishi wetu,
Nyasa.

WAKAZI wanaoishi katika mji mdogo wa Mbamba bay wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, wamesema kwamba hivi sasa tangu kuanza kwa mfungo mtukufu wa mwezi wa Ramadhani wanashindwa  kula kitoweo cha samaki, kutokana na kuuzwa kwa bei ghali tofauti na miezi mingine ya kawaida.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wetu, baadhi ya wakazi hao walidai kuwa hali hiyo inatokana na kutoweka kwa samaki katika ziwa nyasa ambapo hivi sasa hawapatikani kwa urahisi, hivyo wavuvi hutumia  nafasi hiyo kuongeza bei mara dufu zaidi.

Walisema kuwa wilaya ya Nyasa upatikanaji wa mazao mengine ya jamii ya mboga mboga kama vile maharage, kunde, mbaazi na choroko imekuwa ni tatizo ambapo watu wengi hutegemea samaki pekee ikiwa ni mboga ya kila siku katika kuendeshea familia zao.


Hali hiyo walisema wakati mwingine, huwalazimu kutumia mboga mbadala kama vile kisamvu kutokana na uhaba wa tatizo la upatikanaji wa samaki.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake mmoja wa wakazi wa Mbamba bay,  Said Juma alieleza kuwa mbali na kukumbwa na hali hiyo waumini wa dini ya Kiislam kuwa na mahitaji makubwa ya bidhaa mbalimbali ikiwemo samaki, lakini baadhi ya wavuvi wameacha kuendelea na kazi yao ya uvuvi kutokana na kupanda kwa bei ya leseni ya uvuvi kutoka shilingi 10,000 ya awali hadi kufikia shilingi 40,000 kwa mtumbwi mmoja, unaotumika kwa  kazi hiyo ya uvuvi wilayani Nyasa.

Juma alifafanua kuwa halmashauri ya wilaya hiyo, inawatoza kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya kulipia leseni ambacho hakilingani na mapato wanayopata, ambapo alisema hali hiyo inachangia baadhi yao kuachana na kazi hiyo ambayo wanadai haina maslahi kwao.

Naye mkazi mwingine, Samwel Ndomba mkazi wa Njambe wilayani humo alisema ni vigumu kwa sasa kupata samaki wanaoweza kutosheleza mahitaji ya familia zao kwa bei ya chini, kwa sababu ya kupanda kwa bei hiyo ambayo kwa watu wenye kipato cha kawaida wanashindwa kuimudu.

Ndomba alisema kuwa bei ya samaki imepanda kutoka shilingi 1,500 hadi shilingi 3,500 kulingana na ukubwa, huku hata dagaa ambao wanapatikana kwa wingi katika ziwa Nyasa nao bei yake imepanda kutoka shilingi 4,000 hadi shilingi 8,000 kwa dumla (sadolini).

No comments: