Saturday, June 11, 2016

HALMASHAURI YA WILAYA MBINGA MWENGE WA UHURU WAZINDUA MIRADI YENYE THAMANI YA SHILINGI MILIONI 701.6 VIONGOZI WATAKIWA KUTEKELEZA MIRADI YA WANANCHI KWA WAKATI

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya mji wa Mbinga, Oscar Yapesa upande wa kushoto akikabidhi Mwenge wa uhuru jana kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Venance Mwamengo mara baada ya kumaliza mbio zake katika mji wa Mbinga, ambapo Mwenge huo sasa ulikuwa ukiendelea kupelekwa katika miradi mbalimbali ya wilaya hiyo ya Mbinga.


Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

KIONGOZI wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, George Mbijima amewataka viongozi waliopo katika Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, kuhakikisha kwamba fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ya wananchi, zinafanya kazi iliyolengwa ipasavyo ili ziweze kuleta tija katika jamii.

Aidha aliagiza kwamba miradi hiyo inapaswa kutekelezwa kwa wakati, ili kuweza kusaidia kuharakisha mipango mbalimbali ya kimaendeleo ambayo inalenga kuwaondolea umaskini wananchi.

Mbijima alisema hayo jana alipokuwa kwenye ziara ya mbio za Mwenge wa uhuru wilayani humo, ambapo jumla ya miradi saba yenye thamani ya shilingi milioni 701,652,180 Mwenge huo katika miradi hiyo baadhi yake umeweza kufanya kazi ya kuweka mawe ya msingi, kufunguliwa na kuzinduliwa.


Katika miradi hiyo, nguvu za wananchi ni milioni 71,741,400 mchango wa halmashauri ya wilaya milioni 203,000,000 serikali kuu milioni 52,500,000 na taasisi mbalimbali ni milioni 374,410,780.

“Ni wajibu wenu watumishi wa umma kufanya kazi kwa kufuata taratibu na miongozo iliyowekwa na serikali, ili tuweze kufikia malengo tuliyojiwekea na kulifanya taifa letu liweze kusonga mbele kimaendeleo na wananchi waweze kuondokana na umaskini”, alisema Mbijima.

Vilevile aliwataka watendaji hao wa serikali, kutenga maeneo kwa ajili ya vijana kufanyia biashara ikiwa ni lengo la kuwafanya waweze kukua kiuchumi.

Kadhalika alisisitiza kwamba vijana hao, wahamasishwe pia kuunda vikundi vya ujasiriamali ambavyo vitasajiliwa kisheria na kuweza kuwafanya waweze kukopesheka na taasisi za kifedha katika kuendeleza shughuli zao za ujasiriamali.

Pamoja na mambo mengine, kwa mujibu wa risala ya utii wa wananchi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga kwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli ambayo ilisomwa na Mkuu wa wilaya hiyo Senyi Ngaga alisema kuwa tathimini ya mwaka 2015 inaonesha kuwa pato la mwananchi wa wilaya hiyo kwa mwaka, linakadiriwa kuwa ni milioni 2,082,167 ukilinganisha na shilingi 400,000 kwa mwaka 2007.

Lengo la Halmashauri hiyo alisema ni kuongeza pato hilo la sasa na kufikia milioni 2,500,000 ifikapo mwaka 2025 kutokana na wananchi wengi, kuwa na mwitikio mkubwa wa kufanya shughuli za kiuchumi kama vile kilimo cha mazao ya chakula na biashara.

No comments: