Thursday, June 9, 2016

KUSILE RESTAURANT AND LODGE YAFUNGULIWA RASMI NA KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE WA UHURU KITAIFA

Mkurugenzi wa kampuni ya Ovans Construction Company Limited, ambao ni wamiliki wa Kusile Restaurant and Lodge, Valence Urio upande wa kulia akiwa ameshika Mwenge wa Uhuru mara baada ya Kiongozi wa mbio za Mwenge George Mbijima kufungua rasmi hoteli hiyo iliyopo Mbinga mjini mkoani Ruvuma.

Msimamizi wa hoteli ya Kusile Restaurant and Lodge, Mary Thomas upande wa kushoto akisoma taarifa ya maendeleo juu ya ujenzi wa hoteli hiyo ya kisasa kwa Kiongozi wa mbio za Mwenge, George Mbijima wa pili kutoka kulia. Wa pili kutoka kushoto ni mmiliki wa hoteli hiyo, Verena Urio.

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, George Mbijimi akiondoa kitambaa ikiwa ni ishara ya ufunguzi rasmi wa hoteli ya kisasa ya Kusile Restaurant and Lodge iliyopo Mbinga mjini mkoani Ruvuma. (Picha zote na Muhidin Amri Mbinga)
Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

KIONGOZI wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, George Mbijima amefungua mradi wa Hoteli ya kisasa iliyopo Mbinga mjini mkoani Ruvuma kwa lengo la kukabiliana na uhaba wa hoteli unaoukabili mji huo, yenye thamani ya shilingi milioni 110,000,000.

Akisoma taarifa ya mradi huo mbele ya Kiongozi wa mbio hizo za Mwenge, Mary Thomas ambaye ni msimamizi wa mradi huo alisema kuwa mradi huo ambao ni kitega uchumi yaani, “Kusile Restaurant and Lodge” ulibuniwa baada ya kuona mji huo, una tatizo la upatikanaji wa hoteli ya kisasa.

Mary alifafanua kuwa kufunguliwa kwa jengo hilo ni kuunga mkono jitihada za kimaendeleo zinazofanywa na serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais shupavu, John Magufuli katika kutengeneza ajira kwa vijana wa Mbinga na Watanzania wote kwa ujumla ili kuweza kuongeza kipato na kukuza uchumi.

“Ndugu kiongozi wa mbio hizi za Mwenge wa Uhuru, mradi huu umefanikiwa pia kuwawezesha wakulima wadogo wadogo 10 kuanzisha kilimo cha mboga mboga maalumu ambazo hazipatikani hapa Mbinga, hivyo kutengeneza soko la uhakika kwa mboga mboga hizo na zile za kawaida”, alisema Mary.


Pamoja na mambo mengine, alibainisha kuwa katika kutekeleza azma hiyo Kusile hoteli imefanikiwa kutengeneza ajira 22 ambapo kati ya hizo wanawake wapo 16 na wanaume sita.

Kwa upande wake Kiongozi huyo wa mbio za Mwenge, Mbijima aliwataka watoa huduma katika hoteli hiyo wahakikishe kwamba wanatoa huduma zinazolingana na hadhi ya jengo hilo, ili biashara wanazozifanya ziweze kuwa endelevu.

Hata hivyo Mbijima amewapongeza wamiliki wa jengo hilo la biashara, kwa ubunifu walioufanya ambao utasaidia kupunguza uhaba wa nyumba ya kisasa ya kulala wageni na kuweza kupata huduma bora ya chakula.

No comments: