Thursday, June 16, 2016

SENYI NGAGA AWATAKA WATENDAJI MBINGA KUSIMAMIA MAZAO YA WAKULIMA


Na Muhidin Amri,

Mbinga.

WAKULIMA katika kata ya Litumbandyosi wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wameiomba serikali kuandaa sheria kali itakayowabana wafanyabiashara kuacha tabia ya kununua mazao ya wakulima, kwa kutumia vipimo haramu (lumbesa) ambapo hununua kwa bei ndogo isiyolingana na gharama ya uzalishaji.

Senyi Ngaga.
Wakulima hao walisema hayo kwa nyakati tofauti, wakidai kuwa wafanyabiashara hao wamekuwa na tabia ya kwenda vijijini hasa mashambani na kutumia vipimo visivyokubalika kisheria kama vile bakuri na ndoo, kwa ajili ya kununua mazao  kama vile mpunga na mahindi  jambo ambalo huchangia kuwanyonya wakulima na kuwaacha maskini, licha ya kazi kubwa wanayofanya kila mwaka.

Aidha walieleza kuwa kutokana na kuwa na hali ngumu ya maisha ikiwemo suala la upatikanaji wa masoko, wamekuwa wakati mwingine wakilazimika kuuza mazao yao kwa mtindo huo wa vipimo wanavyotumia walanguzi hao ili waweze kujikimu kimaisha ikiwemo suala la kupeleka watoto wao shule.


Theresia Kinyeru ambaye ni mkulima wa zao la mpunga katika kijiji cha Mabuni kata ya Litumbandyosi, alisema wamekuwa wakiteseka na hali hiyo kwa muda mrefu lakini wanashindwa kudhibiti kutokana na wasimamizi wa sheria za vipimo wamekuwa wakikaa mjini, badala ya kwenda vijijini ambako vitendo vingi vya dhuluma vimekuwa vikifanyika.

Alisema wamekuwa wakipata taabu kuanzia hatua ya awali ya maandalizi ya mashamba yao hadi kufikia uvunaji lakini wajanja wachache  wasiokuwa na huruma na mkulima, hutumia mbinu za ujanja kuwanyonya nguvu zao kwa kununua mazao yao kwa bei ndogo.

Kinyeru ameitaka serikali kuwaongeza maafisa vipimo hadi ngazi ya kata, ambao watafanya kazi vijijini hasa  pale kipindi cha msimu wa mavuno ya mazao yao shambani, ili waweze kusimamia vizuri suala hilo kwa ufanisi mzuri.

Mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga, kwa upande wake amewaagiza watendaji wa vijiji na kata kuhakikisha kwamba wanasimamia vyema suala la uuzaji na ununuzi wa mazao ya mkulima ikiwemo kudhibiti wafanyabiashara wanaotumia vipimo visivyokubalika na ambavyo humnyonya mkulima na kumfanya aendelee kuwa maskini.

Ngaga pia alipiga marufuku wafanyabiashara kwenda mashambani kununua mazao ya mkulima, badala yake watumie vituo maalum kama vile maeneo ya siku ya minada ambayo yametengwa kwa ajili ya kazi hiyo, pamoja na kutumia vipimo halisi kama vile mizani zilizopimwa kisheria.

“Nilikwisha waagiza watendaji wangu wote kusimamia jambo hili, tuna upungufu mkubwa wa maafisa vipimo katika wilaya yetu ya Mbinga sasa nimetoa mwongozo watendaji wa vijiji na kata ndiyo watakuwa wasimamizi wa kazi hii, lengo hapa nataka kila mmoja awajibike katika kuchangia uchumi wa nchi yetu”, alisema Ngaga.

No comments: