Saturday, June 11, 2016

KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE APONGEZA HALMASHAURI YA MBINGA USIMAMIZI MZURI KATIKA SEKTA YA ELIMU

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru George Mbijima, akiangalia ubora wa meza na madawati ya kukalia wanafunzi darasani katika kijiji cha Mbuji wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, kabla ya kusambazwa katika shule mbalimbali za msingi na sekondari wilayani humo.

Mratibu elimu kata katika kata ya Litura Halmashauri ya wilaya ya Mbinga vijijini mkoani Ruvuma, Nicodem Hyera akijaribu kuwasha moja kati ya pikipiki zilizotolewa na Halmashauri ya wilaya hiyo kwa ajili ya kuwawezesha Waratibu elimu kata wanaofanya kazi katika mazingira magumu  ziweze kuwasaidia kufuatilia maendeleo ya elimu kwa shule za msingi na sekondari wilayani humo. (Picha zote na Muhidin Amri Mbinga)


Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

HALMASHAURI ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, imepata zawadi ya shilingi milioni 331,252,720 baada ya kukidhi vigezo vitatu vya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo, katika sekta ya elimu wilayani humo.

Vigezo vilivyoifanya halmashauri hiyo iweze kupata tuzo hiyo ni kupanga walimu katika shule zake kulingana na mahitaji husika, kuandaa takwimu za shule zote na kuziweka kwenye mtandao pamoja na kutuma fedha za ruzuku ya uendeshaji kwa wakati kwenye shule husika.

Ofisa elimu msingi wa wilaya hiyo, Samwel Komba alisema hayo wakati alipokuwa akisoma taarifa kwa kiongozi wa mbio za Mwenge wa uhuru Kitaifa, George Mbijima juu ya mikakati ya kukuza elimu katika shule za msingi wilayani humo.


Komba alifafanua kuwa fedha hizo wamezipata kutoka kwa wafadhili wa maendeleo nchi ya Marekani, Uingereza, Sweeden, Benki ya dunia na shirika la Jica ambao wanatekeleza programu inayojulikana kwa jina la Lipa kulingana na matokeo kwa kushirikiana na serikali kuu hapa nchini.

Alisema kuwa wamepewa maelekezo juu ya matumizi ya fedha hizo ambapo ni pamoja na kutenga asilimia tano kwa shughuli za kimaendeleo, kutoa motisha kwa shule na viongozi wa kata wanaohusika na masuala ya elimu.

Hivyo basi katika kutekeleza hilo halmashauri ya wilaya ya Mbinga, imenunua pikipiki mbili zenye thamani ya shilingi milioni 4,700,000 ambazo wamepewa Waratibu elimu kata ya Kitura na Matiri wilayani humo.

“Lengo la kuwapatia pikipiki hizi ni kuweza kuwasaidia kurahisisha kazi za ufuatiliaji shuleni, katika kukuza taaluma na kuboresha miundombinu husika katika shule zetu hapa wilayani”, alisema Komba.

Pia jumla ya shule nane za msingi na sekondari wilayani humo, zimepata mgao wa fedha hizo kwa kupewa kila shule shilingi 200,000 kila mmoja na kufanya jumla ya shilingi milioni 1,600,000.

Shule za msingi za wilaya hiyo ambazo zimepata fedha hizo ni Kitai, Ilela, Longa, Mbugu, Maguu na kwamba kwa shule za sekondari ni Linda, Mkumbi na Mipalu zote zilizopo wilayani Mbinga.

Pamoja na mambo mengine, kwa upande wake kiongozi wa mbio hizo za Mwenge wa uhuru kitaifa, Mbijima alipongeza usimamiaji mzuri unaofanywa katika sekta ya elimu wilayani Mbinga na kuagiza kwamba, uwe endelevu kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye.

No comments: