Tuesday, June 28, 2016

LIKWERA WAENDELEA KUNUFAIKA NA MFUKO WA MAENDELEO YA JAMII

Elimu juu ya matumizi bora fedha za TASAF kwa wananchi imekuwa ikitolewa mara kwa mara kwa wanufaika, ili waweze kuondokana na umaskini. Katika picha ni Justiner Sigera ambaye ni mwezeshaji wa mfuko huo akiwaelimisha hivi karibuni wanufaika wa kijiji cha Mkako wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma.


Na Kassian Nyandindi,

Mbinga. 

KAYA maskini zilizopo katika kijiji cha Likwera kata Nyoni Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wameweza kunufaika na mpango wa kunusuru kaya hizo kwa kupewa fedha shilingi milioni 3,925,000 na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) awamu ya tatu, kwa ajili ya kuendeshea miradi ya ufugaji bora wa kuku, nguruwe na mbuzi.

Husna Chiponda ambaye ni Afisa mtendaji wa kijiji hicho alisema kuwa jumla ya kaya 91 zimewezeshwa fedha hizo, ambazo wamelipwa kwa awamu ya mwisho kwa lengo la kuwawezesha waweze kujikwamua kimaisha na kuondokana na umaskini uliokithiri miongoni mwao.

Aidha aliongeza kuwa kwa upande wa sekta ya elimu, watoto wa shule za msingi wamenunuliwa mahitaji ya shule na kwamba wa sekondari wamelipiwa ada na kupewa mahitaji ya aina mbalimbali, kama vile sare za shule, madaftari na kalamu za kuandikia.


“Watoto 34 wanaosoma sekondari tumewanunulia mahitaji muhimu na kulipiwa ada, kadhalika kwa shule za msingi wapo 19 nao pia tumewapatia mahitaji muhimu”, alisema Husna.

Awali alifafanua kuwa katika awamu iliyopita kaya hizo maskini, ziliwezeshwa shilingi milioni 3,860,000 kutoka pia katika mfuko huo wa TASAF awamu ya tatu katika kijiji hicho cha Likwera.

Husna aliwataka wananchi hao pia kujenga tabia ya kujitokeza katika mikutano pindi wanapotakiwa kufanya hivyo, hasa ikizingatiwa kwamba baadhi yao hata kwenye mkutano wa kuzitambua kaya maskini unapofanyika wamekuwa hawajitokezi jambo ambalo linasababisha wachaguliwe wasio na sifa.

Alifafanua kuwa kwa wale ambao watajiingiza kwenye mpango huo wakati wao sio kaya maskini endapo kama watabainika, wataondolewa mara moja na kwamba aliwaasa wananchi kutoa ushirikiano wa dhati ili mpango huo uweze kufikia katika mafanikio yaliyokusudiwa.

No comments: