Sunday, May 22, 2016

WAKULIMA TUNDURU WATAKIWA KUACHANA NA IMANI ZA USHIRIKINA



Na Steven Augustino,
Tunduru.

WAKULIMA wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wametakiwa kuondokana na tabia za imani ya mambo ya ushirikina kwa madai kwamba wamekuwa wakikosa mavuno katika mashamba yao kutokana na kuchukuliwa kimazingara maarufu kwa jina la Chitola, jambo ambalo limekuwa likiwafanya washindwe kupiga hatua mbele za kimaendeleo.

Aidha kufuatia hali hiyo wameshauriwa kutumia mbinu za kilimo bora, ili waweze kupata mazao mengi shambani badala ya wakati wote kuendekeza imani hizo ambazo hazina faida katika maisha yao ya kila siku.

Katibu tawala wa wilaya hiyo, Ghaibu Lingo ambaye alikuwa akimwakilisha Mkuu wa wilaya ya Tunduru, Agnes Hokororo alisema hayo alipokuwa akizungumza kwenye maadhimisho ya sherehe za siku ya wakulima shambani iliyofanyika katika mashamba darasa ya kilimo cha mahindi na mpunga, yaliyopo kijiji cha Legezamwendo wilayani humo .

Aidha Lingo aliwataka wakulima hao, kuondokana na mila hizo potofu badala yake wawatumie pia wataalamu wa kilimo yaani maafisa ugani, ili waweze kuzalisha mazao yao kwa ubora na viwango vinavyokubalika.


Pamoja na mambo mengine, awali akisoma risala ya maadhimisho hayo Katibu wa kikundi cha wakulima wa mahindi na mpunga, Ahamad Kinunga alisema kuwa wao wamekuwa wakinufaika na utaalamu wa uzalishaji wa mazao hayo kwa ubora unaotakiwa, baada ya kuwatumia muda mwingi wataalamu hao wa ugani chini ya ufadhili wa shirika lisilokuwa la serikali, World Wide Fund for Nature (WWF) chini ya mradi wa kilimo hifadhi.

Alisema kuwa katika kipindi hicho wanavikundi 20 kutoka vijiji vya Legezamwendo, Kidodoma, Machemba na Mkwajuni wilayani hapa walifundishwa kwa vitendo na nadharia juu ya masomo yanayohusu dhana ya shamba darasa na malengo yake ya kuongeza uzalishaji.

Vilevile waliweza kupata elimu juu ya kanuni za kilimo bora, malengo ya mradi wa WWF, kilimo hifadhi, matokeo ya kilimo hifadhi pamoja na uhamasishaji wa uanzishaji wa vikundi hivyo na kufungua akaunti benki.

Akitoa neno la shukrani Diwani wa Kata ya Kidodoma, Rashid Tawala aliipongeza serikali kupitia Halmashauri ya wilaya ya Tunduru kwa kupeleka darasa hilo katika kata yake na akashauri kwamba madarasa hayo, yanapaswa kuwa endelevu kwa manufaa ya jamii katika kata zote za wilaya hiyo.

Naye Meneja wa shirika hilo la WWF mikoa ya Kanda ya Kusini, Nalimi Madata alisema kuwa shirika hilo limelenga kufanya kazi ya uhamasishaji wa shughuli za uhifadhi wa misitu ya asili, ardhi na wanyama pori hapa nchini.

Alisema kuwa liimechukua maamuzi ya kufadhili vikundi vya wakulima wilayani Tunduru, kwa lengo la kuwafanya wakulima hao kuondokana na kilimo cha kuhama hama ikiwa ni juhudi za kuisaidia serikali katika kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.

No comments: