Tuesday, May 3, 2016

SERIKALI YAOMBWA KUTATUA KERO KIGONSERA

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

SERIKALI hapa nchini, imeombwa kufanya jitihada ya kutatua kero ya uchakavu wa miundombinu ya majengo ya shule ya sekondari Kigonsera iliyopo wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, ili kuweza kunusuru yasiweze kubomoka hasa kipindi cha masika ambacho mvua nyingi hunyesha.

Shule hiyo ambayo ilianzishwa mwaka 1938 hivi sasa miundombinu mbalimbali kama vile mabweni ya kulala wanafunzi, vyoo na mabafu ya kuogea yana hali mbaya ambapo yameanza kubomoka kutokana na kutofanyiwa ukarabati kwa muda mrefu.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Hayo yalisemwa na Emmanuel Sayayi mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa wilaya ya Nyasa, Margaret Malenga ambaye alikuwa akimwakilisha Mkuu wa mkoa huo Said Mwambungu katika mahafali yao ya wahitimu kidato cha sita yaliyofanyika shuleni hapo.

Sayayi alisema kuwa shule hiyo ambayo ina historia kwamba aliyekuwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania awamu ya tatu, Benjamin Mkapa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ni miongoni mwa wanafunzi waliosoma shule ya sekondari Kigonsera na kwamba, licha ya kuwepo kwa changamoto hizo shule hiyo pia ina upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi jambo ambalo linasababisha baadhi yao kutomaliza mihtasari ya masomo kwa wakati.

Alifafanua kuwa serikali iongeze walimu wa masomo hayo, ikiwemo na zana za kujifunzia vitabu vya ziada, maktaba na vifaa vya maabara hasa kemikali na gari kwa ajili ya usafiri ili kuweza kutatua changamoto ya ukosefu wa kukosa kushiriki ziara mbalimbali za kitaaluma, michezo na malezi.


“Tunaiomba pia serikali iingize shule yetu kwenye mpango wa ruzuku ya mbolea na mbegu za mahindi, ili tuweze kuboresha mradi wetu wa shamba la mahindi na kadhalika iwekwe kwenye mpango wa kupewa ruzuku ya mafuta ya kuendeshea jenereta letu au shirika la ugavi wa umeme Tanzania (TANESCO) lituletee miundombinu ya umeme, tuweze kuondokana na kero ya upatikanaji wa nishati hii muhimu”, alisema Sayayi.

Pamoja na mambo mengine, akihutubia kwenye mahafali hayo Mkuu wa wilaya ya Nyasa Margaret Malenga alisema kuwa shule hiyo ambayo inahistoria nzuri ya kutoa viongozi mashuhuri hapa nchini, hivyo kwa mujibu wa maagizo yaliyotolewa na Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Mwambungu, kwamba amemtaka Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani humo, Venance Mwamengo ahakikishe anaomba kibali kwa Waziri Mkuu kitakachomfanya aweze kununua gari jipya na kulikabidhi kwa uongozi wa shule hiyo.

Akizungumzia juu ya suala la upatikanaji umeme shuleni hapo, amemtaka pia Mkurugenzi huyo kukaa pamoja na Meneja wa TANESCO wa wilaya hiyo na kuona namna gani wanamaliza kero hiyo ya kupeleka miundombinu ya umeme shuleni hapo ili wanafunzi hasa wa masomo ya sayansi, waweze kusoma masomo yao darasani kwa ufanisi mzuri.


Malenga aliongeza kuwa kuhusiana na suala la upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi ameutaka uongozi wa sekta ya elimu mkoani humo, kuweka kipaumbele katika ajira mpya ya walimu kuhakikisha kwamba walimu watakaoajiriwa, baadhi yao wapelekwe kwanza katika shule ya sekondari kigonsera ili kuweza kukabiliana na tatizo hilo la upungufu wa walimu huku suala la ukarabati wa majengo ya shule hiyo, alisema atalifikisha kwa uongozi husika serikalini ili kuweza kuona ni namna gani linapatiwa ufumbuzi wa haraka.

No comments: