Monday, December 15, 2014

DEREVA ALIYEFANYA MAUAJI TUNDURU ASAKWA



Na Steven Augustino,
Tunduru.

POLISI wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wanamsaka dereva aliyekuwa akiendesha pikipiki aina ya SUNLG yenye namba za usajiri T 115 CZE ili aweze kujibu mashitaka ya mauaji aliyoyafanya baada ya kumgonga mwendesha baiskeli.

Dereva huyo ambaye jina lake halijafahamika anadaiwa kufanya mauaji hayo, Disemba 13 mwaka huu majira ya saa 5:00 asubuhi katika kijiji cha Tuleane kilichopo Tarafa ya Mlingoti – Namasakata mjini hapa.

Imeelezwa na Kamanda wa polisi wa mkoa huo, Mihayo Msikhela kuwa mauaji hayo aliyafanya kwa kumgonga na pikipiki Rashid Tawakali (50) wa kijiji cha Nakayaya wilayani humo na kumsababishia kifo papo hapo.


Msikhela alisema baada ya mtuhumiwa kufanya tukio hilo ametokomea kusikojulikana, na kuitelekeza pikipiki hiyo katika eneo la tukio baada ya kumgonga mwendesha baiskeli huyo na kusababisha kifo chake.

Alisema baada ya tukio hilo mwili wa marehemu ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti kilichopo katika hospitali ya serikali wilayani Tunduru na baadae ndugu wakafanikiwa kuutambua mwili wake na kuruhusiwa kwenda kumzika.

Kamanda Msikhela ametoa wito kwa wananchi wanaojua taarifa zozote juu ya mmiliki au dereva wa pikipiki hiyo, kuwasaidia ili kuwezesha kumkamata na sheria iweze kuchukua mkondo wake.

No comments: