Wednesday, December 3, 2014

KILELE CHA MAADHIMISHO YA WALEMAVU IRINGA: SERIKALI YAPIGA MARUFUKU UJENZI WA MAJENGO YASIYO RAFIKI KWA WALEMAVU


Waziri  wa nchi  ofisi ya  waziri  mkuu (sera na uratibu wa bunge) William Lukuvi akihutubia katika kilele  cha siku ya  walemavu duniani, maadhimisho  yaliyofanyika katika viwanja vya kichangani mjini Iringa Kitaifa,  na Lukuvi kumwakilisha  Waziri mkuu Mizengo Pinda ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo.


Waziri  wa nchi  ofisi ya  waziri mkuu  sera  na uratibu wa bunge, William Lukuvi akimkabidhi cheti cha ushiriki mlemavu, Tumaini  Mdegella kwa  niaba ya ofisi za Neema Crafti mjini Iringa  wakati wa kilele  cha maadhimisho ya  siku ya  walemavu duniani, yaliyofanyika kitaifa  mjini humo.
Na Mwandishi wetu,
Iringa.

SERIKALI  imeziagiza  Mamlaka  za  usafiri  wa majini na nchi kavu (SUMATRA )  nchini,  kuanza mchakato  wa  kukaa na  wamiliki wa  vyombo  hivyo  ili kuanza  uagizaji  wa vyombo  vya usafiri yakiwemo mabasi ambayo ni  rafiki na walemavu nchini, huku ikipiga marufuku  majengo ya   serikali kujengwa bila kuwepo kwa  mchoro  unaoonyesha mazingira yanayozingatia makundi  yote ya jamii  likiwemo la walemavu wa viungo.

Agizo   hilo  limetolewa na  Waziri  mkuu Mizengo  Pinda, wakati  wa maadhimisho ya  siku ya  walemavu  duniani yaliyofanyika   kitaifa  katika  viwanja  vya kichangani mkoani  Iringa.

Akiwahutubia   walemavu hao na  wananchi  waliofika katika  viwanja   hivyo waziri  mkuu, aliyewakilishwa na Waziri  wa nchi  ofisi ya  waziri mkuu (sera na uratibu wa bunge) Wiliam Lukuvi ambaye ni mbunge wa  jimbo la Isimani mkoani Iringa, alisema kimekuwepo kilio  cha muda  mrefu kutoka kwa  walemavu  juu ya kusahulika katika ujenzi  wa  majengo mbalimbali, ambayo yamekuwa  yakijengwa  bila kuzingatia  kundi la  watu  wenye  ulemavu jambo ambalo ni sawa na  kuwabagua watu  hao.

Aidha alisema  katika  kuona kilio  hicho  cha  walemavu  kinafanyiwa  kazi  kuanzia  sasa, majengo  yote ya  serikali  zikiwemo  shule na taasisi nyingine  kabla ya  kuanza  ujenzi  wake lazima  wasimamizi wa  ujenzi  huo kujiridhisha kwa  mchoro ambao  utaonyesha  mazingira  yatakayomuwezesha  mlemavu,   kutumia jengo  husika bila usumbufu  wowote tofauti na  ilivyo sasa ambapo  idadi kubwa ya majengo mazingira  yake  si rafiki kwa  mlemavu.

"Ni  siku  nyingi  watu  wenye ulemavu  wamekuwa  wakilalamika juu ya mazingira  yasiyo rafiki    katika majengo  mbalimbali............ sasa  leo naomba  kuagiza  kuwa michoro yote inayochorwa katika majengo ya  huduma za  kijamii,  ni marufuku  kupitishwa ama  wasimamizi  wa  ujenzi  husika  kuruhusu ujenzi  iwapo mchoro hauonyeshi  kama utajali makundi  yote wakiwemo  walemavu,

“Wasimamizi  wote msikubali  kusimamia  wala  kutangaza  tenda  ya ujenzi kama ramani  yake  si rafiki kwa  mlemavu, lakini  pia  hata  kwenye mabasi hivi unamtegemea mtu mwenye ulemavu wa miguu ataingia vipi na baiskeli  yake  katika gari iwapo hakuna mazingira  yanayomwezesha  kuingia, hivi  sasa  teknlojia  imezidi kukua na baadhi ya nchi  wameanza muda mrefu kuwajali walemavu kwa kuwa na mabasi ambayo mlemavu anaingia na baiskeli  yake  na  kushuka nayo   bila usumbufu, ni vyema hata Sumatra mkaangalia uwezekano wa  kuwajali  walemavu hawa”, alisema  Lukuvi.


Kuhusu  ombi la walemavu hao   hasa  kwa wale  wasiosikia wameiomba  serikali  kuwa na wakalimani katika kituo cha Televisheni ya  Taifa (TBC) na vituo  vingine  vya  luninga,  ili  kuwawezesha  walemavu hao nao  kuweza  kufuatilia hotuba  ya Rais mwisho  wa mwezi na mambo mengine badala ya  kutengwa.

Lukuvi alisema  kuwa  suala  hilo  ni  wajibu wa  serikali  kuwajali  watu  wake  hivyo tayari  imeuagiza  uongozi  wa TBC, na mamlaka ya  mawasiliano Tanzania (TCRA)  kulitafutia  ufumbuzi  suala  hilo la  mkalimani  hasa katika TBC .

Katika  hatua nyingine  Lukuvi  aliwataka  walemavu hao  ili  ombi lao la  kutazamwa katika  nafasi za  uongozi  liweze  kuzingatiwa, ni  vyema  wao  wenyewe  kujitokeza kwa  wingi  kuipigia  kura  katiba  iliyopendekezwa pindi  itakapokuja kwa  wananchi kwa madai kuwa  katika  katiba   hiyo imezingatia mambo  mengi ya kijamii, likiwemo la  kuwajali  watu  wenye ulemavu kwa  kuwatengea nafasi nyingi  zaidi  na  iwapo  katiba  hiyo  itapitishwa kazi ya msuguano wa  rushwa unaweza  kuhamia kwa  walemavu kwa kila mmoja kutaka  kupewa nafasi.

"Hadi  hivi  sasa ni chama cha mapinduzi (CCM) pekee ambacho  kina wabunge wa viti maalum wa  kuteuliwa  kutoka kundi la  walemavu huku  vyama  vingine  vyote  havijawakumbuka kabisa  watu  wenye ulemavu ukiacha  mbunge wa  jimbo la Lindi mjini pekee ambae hakupendelewa  katika ubunge  wake bali alishindwa kihalali kwa  kuchaguliwa na  wananchi  wake..nafikiri  tushirikiane  kuhakikisha katiba  hii iliyopendekezwa  inapita  ili  tuungane pamoja katika  kujenga nchi  yetu”, alisema.

Katika  salaam  za  walemavu kote nchini, Waziri  wa Afya  na ustawi  wa jamii  Dokta Seil Rashid  zilizotolewa kwa  niaba  yake  na mwenyekiti  wa baraza la  watu  wenye ulemavu nchini na Dunford Makala,   alisema  kuwa  wizara  inaendelea   kuimarisha  ushirikiano na vyama  vya  watu wenye ulemavu,  na  shirikiasho  la vyama  vya  watu  wenye ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) katika  kuhakikisha utekelezaji  wa uwekaji  wa fursa  na haki  sawa  kwa  watu  wenye ulemavu nchini.

Alisema  katika  kuhakikisha ushirikiano unakuwepo  wizara yake  imezindua baraza  la  ushauri  la Taifa  la  watu  wenye  ulemavu,  toka mnamo 1  Novemba 2014 na katika  hilo  kamwe  hawataacha  kumpongeza  Rais Dokta Jakaya Kikwete  kwa   kumteua  mwenyekiti  wa baraza hilo.

Alifafanua kuwa ni ukweli  usiopingika kuwa nchi  hii chini ya Rais Dkt  Kikwete  imefanya mambo  mengi  zaidi ya  kuwajali  watu  wenye  ulemavu  katika Nyanja  za  kiuchumi, kiutamaduni na  kisiasa ambavyo  vyote  hivyo  kumwezesha  mlemavu kujikwamua  kimaisha.

Hata   hivyo  alisema  ushahidi  wa yote hayo ni pamoja na kuridhia mikataba  ya kimataifa  juu ya haki  za watu wenye ulemavu, kutungwa kwa sheria Na.9 ya mwaka 2010 ya watu  wenye ulemavu  na kanuni zake, kuwashirikisha  watu wenye ulemavu  katika tume ya mabadiliko ya katiba  ya Jamhuri ya  Muungano wa Tanzania pamoja na kuteuliwa kwa  wajumbe 20  wenye ulemavu  katika  bunge maalumu la mabadiliko ya katiba la mwaka 2014.

Awali  walemavu hao  katika  risala yao  iliyosomwa na makamu  mwenyekiti  wa SHIVYAWATA  Amina Mollel, pamoja na  kuishukuru  serikali kwa jinsi  kwa  kuendelea  kuwa karibu  zaidi na  watu  wenye ulemavu kwa kushiriki shughuli mbali mbali za  walemavu, bado waliweza  kuishukuru  serikali kwa kuandaa sera ya maendeleo ya  watu wenye ulemavu ya mwaka 2004, kutambuliwa  kwa  watu wenye ulemavu katika MKUKUTA, kuwezesha kuongezeka kwa idadi ya watu wenye ulemavu  wanaopata  elimu kuanzia shule za msingi hadi elimu ya juu na mambo  mengine  mengi ambayo  wao kama  walemavu wamekuwa  wakiona  serikali  yao  ipo pamoja nao.

Sanjari na mema  hayo bado  waliiomba serikali kuzingatia kuwapatia  walemavu mambo muhimu katika maisha ya kila  siku ikiwa ni pamoja na kuwa na vyombo  vya usafiri rafiki kama magari  moshi.vyombo  vya usafiri majini ,angani ,miundo mbinu katika  majengo  na viwanja  vya  ndege ambavyo  vitamwezesha mlemavu pia kuwa  huru.

Mkuu  wa mkoa wa Iringa Amina Masenza  alisema  kuwa maadhimisho hayo yaliyofanyika  chini ya kauli  mbiu  isemayo, "Maendeleo endelevu ahadi  ya Teknolojia,  huku mkoa  wa  Iringa  ukiendelea  kuwa  bega kwa  bega  na  walemavu ikiwa ni pamoja na  kufanya kazi karibu na  vyama  hivyo  vya  watu  wenye  ulemavu   na kuwa mkoa huo  kwa  sasa, una jumla ya  walemavu  zaidi ya 179,000 na  wote  serikali  imeendelea  kuwalinda na  kuwa nao pamoja.


No comments: