Sunday, December 28, 2014

KWA MABOMU HAYA YA SONGEA, TUNAPASWA KUJIULIZA VYOMBO VYA ULINZI NA USALAMA VIPO WAPI?

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu.
Na Kassian Nyandindi,

MATUKIO ya mabomu mjini Songea hapa mkoani Ruvuma, umekuwa sasa ni mchezo mchafu ambao unahatarisha usalama wa raia, hivyo kuna kila sababu kwa serikali kuchukua hatua madhubuti juu ya kudhibiti hali hii.

Tunasema kuna kila sababu sasa ya kufanya hivyo, kutokana na kile tunachoweza kusema kwamba tumechoka kusikia kauli za viongozi wa ngazi ya juu hususani hapa mkoani, wakisema kwamba watahakikisha hali hii itadhibitiwa kwa kuwakamata wahusika ili matukio kama haya yasiweze kuendelea kutokea.

Ni muhimu sasa kuona namna gani tunashirikisha jamii kwa karibu zaidi, ili waweze kutoa ushirikiano wa kutosha ambao baadaye utaweza kuleta tija katika kukomesha genge la watu hawa, ambao wanahusika kutengeneza mabomu haya.

Hili ni tukio la tatu sasa kutokea hapa songea, mara ya kwanza askari polisi walirushiwa bomu, mara ya pili lilitegwa karibu na kituo cha kurusha matangazo (TBC) mjini Songea na leo askari hawa hawa wanarushiwa tena, tunapenda kuhoji vyombo vya ulinzi na usalama vipo wapi au vimeenda likizo? 

Tunahoji hivyo sio kwa nia mbaya, kwa sababu mara kwa mara tumekuwa tukiwanukuu baadhi ya vigogo wakisisitiza na kuahidi kukomesha hali hii isiweze kuendelea kutokea, lakini inashangaza kuona matukio haya yanajirudia na kuwafanya watu waishi kwa wasiwasi.


Leo Songea imefikia hatua ya kulipuliwa mabomu, yatupasa sasa viongozi husika tuache kukaa maofisini na kuishia kusoma mafaili tu, twendeni huku na kule tukachunguze ili tuweze kukomesha hali hii ambayo inahatarisha usalama wa raia wetu.

Mara kwa mara timu ya wataalamu wa kuchunguza mambo tumeshuhudia ikiundwa, lakini hatma ya kazi wanayofanya hatuoni kuzaa matunda ipasavyo ndio maana genge la wahuni ambao wanamazoea ya kutengeneza mabomu, wamekuwa wakiendelea kutamba na kujeruhi askari wetu ambao hawana hatia.

Katika kuyasemea haya nashauri pia ulinzi uimarishwe pande zote za mkoa wetu wa Ruvuma, hata sehemu zenye mipaka ambayo tumepakana na nchi jirani huenda wahalifu hawa wakatokea huko na kuja kuleta vurugu hizo, ambazo zina hatarisha ustawi wa maendeleo katika mkoa wetu na taifa kwa ujumla.

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu wewe ndiye baba yetu na Mwenyekiti wa Kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa huu, ni wakati sasa wa kuhakikisha unapambana ipasavyo juu ya matukio haya, ambayo yanaharibu na kuchafua sifa ya mkoa wetu.

Tunategemea siku moja genge hili la wahuni wanaozalisha mabomu na kujeruhi askari wetu, litafahamika na kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwemo hata kufungwa jela maisha ili kuwatokomeza kabisaaa………. na wasionekane tena wakiranda randa mitaani na kuhatarisha usalama wetu.

Nasema ifike mahali hakuna haja ya kulala usingizi tena, tuchape kazi usiku na mchana ili tuweze kubaini kiini cha shetani huyu wa mabomu kipo wapi hapa kwetu mkoani Ruvuma na tukisha baini ukweli ni wapi wapo, hatua zichukuliwe haraka iwezekanavyo.
Mwenyezi Mungu ibariki Tanzania na mkoa wetu wa Ruvuma!

Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa barua pepe,        nyandindi2006@gmail.com.

No comments: