Wednesday, December 3, 2014

WAZIRI MKUU PINDA MBINGA KUNA HAJA YA SERIKALI KUINGILIA KATI KUMALIZA TATIZO HILI

Waziri Mkuu Mizengo Pinda.

Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

TAARIFA ya Mkaguzi wa ndani juu ya hoja zilizojitokeza katika kikao cha fedha, mipango na uongozi kilichoketi Septemba 25 mwaka huu wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, na kuwasilishwa katika kikao cha baraza la madiwani la wilaya hiyo Oktoba 27 mwaka huu, imeendelea kukosolewa na wadau mbalimbali wa elimu wilayani humo wakisema kwamba ni mpango mbovu ambao ulisukwa na watu wachache wenye ni mbaya ya kurudisha nyuma maendeleo katika sekta ya elimu, licha ya kila kilichoelezwa kwenye taarifa hiyo kilikwishapitishwa kwenye vikao halali vya halmashauri ya wilaya hiyo.

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo Hussein Ngaga ndiye anayenyoshewa kidole akidaiwa kuwa na kundi la watu wachache, ambao wanaelezwa ndiyo vinara wa kusuka mpango huo ambao sasa umefikia katika hatua ambayo inaleta mgogoro ambao hauna tija kwa wanambinga.

Ngaga katika taarifa hiyo ametoa hoja saba za kumtuhumu Afisa elimu wake wa idara ya elimu msingi Mathias Mkali kwamba, amefanya ukiukwaji mkubwa wa sheria, kanuni na taratibu za fedha za utumishi wa umma, jambo ambalo tumelifanyia utafiti na kubaini sio kweli badala yake ni mambo ambayo yalikwisha kubaliwa na kupitishwa kwenye vikao halali. (nakala tunazo) 

Katika hali ya kushangaza, taarifa hiyo iligawiwa kwa madiwani katika baraza hilo ambayo imesainiwa na mkurugenzi huyo, ghafla Wajumbe husika (Madiwani) baada ya taarifa hiyo kumaliza kusoma mkaguzi wa ndani, Laston Kilembe walinyang’anywa huku mkurugenzi akisimama mbele ya kikao na kueleza kuwa haijakamilika watapatiwa tena katika kikao kijacho cha baraza hilo.

Hali hiyo iliyojitokeza wengi wao walikuwa wakihoji inakuwaje baraza linaletewa taarifa ambayo haijakamilika, huku wengine wakisema huenda ndio ulikuwa mpango wenye kubeba matakwa binafsi ambayo hayana tija kwa jamii.


Walisema kuwa wanachotambua siku zote, jambo ambalo limefanyiwa upembuzi yakinifu na kufikia maamuzi ya kutolewa katika baraza la madiwani maana yake ni kwamba, lilikwisha kamilika katika kufanyiwa kazi na sio kulileta nusunusu kitendo ambacho kinatia shaka kati ya utendaji kazi wa mkurugenzi mtendaji na mkaguzi wake wa ndani kwa kile kinachoelezwa kuwa, huenda ni mpango wao binafsi wenye kutaka kuharibu mwenendo na makubaliano husika ambayo yalikwisha pitishwa kwenye vikao halali.

Walifafanua kuwa ni vyema mkaguzi wa ndani Bw. Kilembe akafanya kazi kwa misingi yenye kujali maslahi ya taifa, kama miongozo yake ya kazi inavyomtuma na sio kutoa taarifa ambazo hazijakamilika na zenye kuleta sintofahamu ambayo baadaye huleta shida na kujenga makundi yasiyokuwa ya lazima.

Utafiti uliofanywa na mwandishi wa habari hizi umebaini kuwa, hoja za mkaguzi huyo wa ndani hazina mashiko, huku ikibainika kuwa tuhuma nyingi alizozitoa mbele ya baraza hilo ni makubaliano ambayo yalikwisha pitishwa na kuridhiwa  katika vikao halali vya baraza la madiwani.

Kilembe katika kikao hicho cha baraza la madiwani, alizua gumzo ndani ya baraza hasa pale baadhi ya madiwani walipohoji kuwa taarifa yake kwa nini haina majibu ya upande wa pili wa mtuhumiwa, yaani Afisa huyo wa elimu msingi wa wilaya ya Mbinga Bw. Mkali.
Walisema, kutoa kwa taarifa yake ya upande mmoja ambayo haina majibu ya upande wa pili wa mtuhumiwa, ni kutotenda haki na ndio maana madiwani walishindwa kuunga mkono na kubakia kuleta gumzo ndani ya baraza.

Katika kikao hicho cha baraza la madiwani hata Katibu tawala wa wilaya ya Mbinga Stephano Ndaki na mkurugenzi wake Hussein Ngaga, kwa nyakati tofauti walinukuliwa wakisema kwamba suala hilo litaundiwa tume ya uchunguzi jambo ambalo utekelezaji wake haujafanyika hadi sasa, huku baadhi ya wadau wakiendelea kuhoji na kusema kauli zao ndani ya baraza hilo zilikuwa ni danganya toto na maneno ya kupumbaza watu.

Hata hivyo endelea kufuatilia mtandao huu tutachapisha taarifa yote ya mkaguzi huyo wa ndani, ambayo ilisomwa katika baraza na imesainiwa na mkurugenzi huyo na baadaye Madiwani walinyang’anywa kwa madai kwamba haikukamilika, huku wengi wakihoji kama haikukamilika kwa nini ililetwa kwenye baraza hilo na kuwasilishwa.

No comments: