Saturday, December 27, 2014

JESHI LA POLISI NCHINI LAUNDA TIMU KUCHUNGUZA TUKIO LA BOMU SONGEA

Askari aliyejeruhiwa na bomu mjini Songea mkoa wa Ruvuma, WP Mariamu Lukindo akiwa amelazwa katika hospitali ya mkoa huo iliyopo mjini hapa.
Na Mwandishi wetu,
Songea.

TIMU ya makachero kutoka makao makuu ya Jeshi la polisi nchini, wakishirikiana na wa mkoa wa Ruvuma, kwa ajili ya kufanya uchunguzi kuhusiana na matukio ya mabomu yanayoendelea kujitokeza mara kwa mara mkoani humo.

Makachero hao wanatoka Jijini Dar es salaam, kufanya uchunguzi kuhusiana na tukio la mtu mmoja aliyelipukiwa na bomu maeneo ya majengo mjini songea  na kujeruhi askari polisi wawili, wakati akijiandaa kuwarushia  askari waliokuwa doria na kisha bomu hilo kumuua mwenyewe.

Hayo yalisemwa na kaimu mkurugenzi wa makosa ya jinai nchini, Naibu Kamishna wa Jeshi la Polisi Diwani Athumani aliyewasili mjini  Songea kwa helkopta kwa ajili ya tukio hilo ambalo mtu ambaye hajatambulika,   amelipukiwa na bomu hilo na kufariki dunia  papo hapo wakati akijaribu kuwarushia askari waliokuwa doria na kujeruhi askari wawili.

Aliwataja askari waliojeruhiwa kuwa ni PC Mselemu na WP Mariamu Lukindo  ambaye bado amelazwa katika hospitali ya mkoa iliyopo mjini Songea.


Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said  Mwambungu aliyemtembelea majeruhi Mariamu Lukindo, ameeleza kusikitishwa na tukio hilo ambalo ni la tatu kutokea mwaka huu mjini hapa, likiwalenga  askari polisi.

Nao wananchi wanaoishi jirani na ulipotokea mlipuko  wa bomu hilo, wameeleza hofu waliyokuwa nayo baada ya mlipuko huo wa bomu na kuitaka serikali kufanya jitihada ya kudhibiti hali hiyo ambayo inaendelea kuleta hofu kubwa kwa raia, juu ya maisha na mali zao.

Mtu mmoja ambaye hajatambulika jina lake na anakotoka amefariki dunia baada ya kulipukiwa na bomu huku utumbo wake ukiwa nje, na mkono wake kukatika alipotaka kuwarushia askari hao.

Mkuu huyo wa mkoa wa Ruvuma alisema kuwa watu wa nne waliokuwa na mtu huyo aliyekuwa akirusha bomu hilo, wamekimbia huku polisi wakikamata simu za watu hao pamoja na ya marehemu huyo.

Mwambungu alisema kukamatwa kwa simu hizo ni mwanzo mzuri wa kuwabaini walipuaji mabomu kwa askari polisi mjini Songea.

No comments: