Saturday, July 2, 2016

VIONGOZI MKOA WA NJOMBE WANYOSHEWA KIDOLE KWA KUFUMBIA MACHO MALALAMIKO YA WANANCHI



Na Kassian Nyandindi,

Njombe.

DIWANI wa kata ya Mbalatse wilayani Makete mkoa wa Njombe, Edson Msigwa amesema kwamba amechukizwa na kitendo cha viongozi wa mkoa huo kufumbia macho kwa muda mrefu malalamiko ya wananchi wake, juu ya kutwaliwa ardhi yao na mwekezaji wa Kampuni ya Silverlands Tanzania yenye makao yake makuu mkoani Iringa bila kufuata taratibu husika, jambo ambalo linahatarisha kutokea kwa machafuko kati ya wananchi na mwekezaji huyo.

Mkuu wa mkoa wa Njombe, Dkt. Rehema Nchimbi.
Msigwa ambaye ni diwani wa kata hiyo, kupitia tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) alisema kuwa licha ya kero hiyo kufikishwa mezani kwa viongozi wa ngazi ya mkoa huo hakuna hatua zinazoonesha kuzaa matunda hivyo kuna kila sababu kwa serikali, kuchukua hatua za haraka ili kuweza kunusuru hali hiyo isiweze kuleta madhara hapo baadaye.

Hayo yalisemwa na diwani huyo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ambao walitembelea katika kata ya Mbalatse, kwa lengo la kutaka kujua juu ya hatma ya mgogoro wa ardhi ambao umedumu kwa muda mrefu kati ya wananchi na mwekezaji huyo.

Alisema kuwa tangu mwaka 1980 mwekezaji huyo aliingia katika kata ya Mbalatse kwa ombi la kupewa ardhi ekari 70 ili aweze kufanya utafiti wa kilimo cha zao la shairi, lakini anashangaa kuona kwamba amemilikishwa eneo la zaidi ya hekta zaidi ya 3,000 bila kufuata taratibu za uchukuaji wa maeneo ya wananchi wake kama sheria za nchi zinavyotaka.


“Wananchi wa Mbalatse wanajua kwamba ardhi yao inatumika kwa manufaa ya watu binafsi sio kwa manufaa ya taifa, hivyo kupokwa kwa ardhi hii zimetumika njia za hila na udanganyifu mkubwa”, alisema Msigwa.

Alifafanua kuwa hata uongozi wa kata hiyo haujui chochote kinachoendelea katika mashamba hayo kufuatia ulinzi mkali ambao umewekwa na mwekezaji, ambapo walinzi waliopo muda wote usiku na mchana wamekuwa na silaha za moto ili kuzuia mtu yeyote asiweze kuingia katika eneo hilo. 

Kadhalika Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Makete Egnatio Mtawa alipohojiwa na waandishi wa habari, alikiri kuwepo kwa mgogoro huo na kuongeza kuwa tayari hatua zimeanza kuchukuliwa tume imeundwa kuchunguza kwa undani juu ya jambo hilo, ambapo baadaye itatoa taarifa baada ya kumaliza kazi yake.

Naye Meneja wa shamba la kampuni ya Silverlands Tanzania, Steven Maina wa eneo la Mbalatse alipoulizwa juu ya jambo hilo alikanusha na kusema kuwa hakuna mwananchi yeyote aliyewahi kwenda ofisini kwake na kutoa malalamiko hayo, huku akiongeza kuwa kama kuna mtu anataka kufahamu juu ya umiliki wa shamba hilo awasiliane na uongozi wa kampuni hiyo na sio vinginevyo.

Hata hivyo Mkuu wa mkoa wa Njombe, Dkt. Rehema Nchimbi alipotakiwa kutolea ufafanuzi juu ya hali hiyo aliwataka waandishi wa habari kwenda kumuona Afisa mipango miji wa mkoa huo Sarah Seme, ambapo baada ya kuonana naye alikanusha uwepo wa mgogoro huo wa ardhi katika kata ya Mbalatse na kuongeza kuwa wananchi wa kata hiyo wanataka shamba hilo linaloendeshwa na mwekezaji huyo lirejeshwe mikononi mwao, ili waweze kuzalisha mazao yao ya aina mbalimbali.

No comments: