Monday, July 18, 2016

MBUNGE MAKETE ASIKITISHWA NA UONGOZI WA MKOA KUFUMBIA MACHO TATIZO LA MGOGORO WA ARDHI

Wananchi wa kata ya Mbalatse wilayani Makete mkoa wa Njombe, wakiwa wameandamana kutaka ardhi yao iliyochukuliwa na mwekezaji. (Picha kwa hisani ya ITV)


Na Kassian Nyandindi,

Njombe.

MBUNGE wa Jimbo la Makete mkoa wa Njombe, Profesa Norman Sigala amesema kwamba anasikitishwa na kitendo cha uongozi wa mkoa huo kufumbia macho kwa muda mrefu malalamiko ya wananchi wake, juu ya kutwaliwa ardhi yao na mwekezaji wa kampuni ya Silverlands Tanzania bila kufuata taratibu husika, jambo ambalo linahatarisha kutokea kwa machafuko kati ya wananchi na mwekezaji huyo.

Mbunge huyo ambaye ni wa kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) alisema kuwa licha ya kero hiyo kufikishwa mezani kwa viongozi wa ngazi ya mkoa huo hakuna hatua zinazoonesha kuzaa matunda hivyo kuna kila sababu kwa serikali, kuchukua hatua za haraka ili kuweza kunusuru hali hiyo isiweze kuleta madhara hapo baadaye.

Hayo yalisemwa na Profesa Sigala alipohojiwa na waandishi wa habari ambao walitembelea katika kata ya Mbalatse wilayani Makete, kwa lengo la kutaka kujua juu ya hatma ya mgogoro wa ardhi ambao umedumu kwa muda mrefu sasa kati ya wananchi na mwekezaji huyo.


Alisema kuwa tangu mwaka 1980 mwekezaji huyo aliingia katika kata ya Mbalatse kwa ombi la kupewa ardhi ekari 70 ili aweze kufanya utafiti wa kilimo cha zao la shairi, lakini anashangaa kuona kwamba amemilikishwa eneo la hekta zaidi ya 3,000 bila kufuata taratibu za uchukuaji wa maeneo ya wananchi wake kama sheria za nchi zinavyotaka.

“Nasikitishwa sana na kitendo kinachofanywa na uongozi huu wa mkoa kutoshughulikia mgogoro huu wa ardhi ili uweze kwisha kwa wakati na madhara yasiweze kutokea hapo baadaye, wananchi wa Mbalatse wanajua kwamba ardhi yao inatumika kwa manufaa ya watu binafsi sio kwa manufaa ya taifa, hivyo kupokwa kwa ardhi hii zimetumika njia za ujanja ujanja na udanganyifu mkubwa”, alisema.

Naye Diwani wa Kata ya Mbalatse, Edson Msigwa alifafanua kuwa hata uongozi wa kata hiyo haujui chochote kinachoendelea katika mashamba hayo kufuatia ulinzi mkali ambao umewekwa na mwekezaji huyo, ambapo walinzi waliopo muda wote usiku na mchana wamekuwa na silaha za moto ili kuzuia mtu yeyote asiweze kuingia katika eneo hilo.

Kadhalika Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Makete Egnatio Mtawa alipohojiwa, alikiri kuwepo kwa mgogoro huo na kuongeza kuwa tayari hatua zimeanza kuchukuliwa tume imeundwa kuchunguza kwa undani juu ya jambo hilo, ambapo baadaye itatoa taarifa baada ya kumaliza kazi yake.

Naye Meneja wa shamba la Kampuni ya Silverlands Tanzania, Steven Maina alipoulizwa juu ya jambo hilo alisema kuwa ndani ya eneo hilo wao wana hati miliki na kwamba kuna kiwanja cha ndege ambacho kimekuwa kikitumika ndege kutua kipindi cha kiangazi, wakati wa mavuno ya zao hilo na kwamba pia kumejengwa majengo ya ofisi na nyumba za kuishi wafanyakazi wa shamba hilo.

Maina alifafanua kuwa sehemu ya shamba hilo kumezalishwa pia zao la shairi alizeti, ngano na mboga mboga pamoja na miti ya asili na kwamba haoni sababu ya mgogoro huo kuendelezwa huku akishauri kwamba kuna kila sababu ya serikali kuchukua hatua ya kumaliza tofauti zilizopo.

Hata hivyo Mkuu wa mkoa wa Njombe, Dkt. Rehema Nchimbi alipotakiwa kutolea ufafanuzi juu ya hali hiyo aliwataka waandishi wa habari kwenda kumuona Afisa mipango miji wa mkoa huo Sarah Seme, ambapo baada ya kuonana naye alikanusha uwepo wa mgogoro huo wa ardhi katika kata ya Mbalatse na kuongeza kuwa wananchi wa kata hiyo wanataka shamba hilo linaloendeshwa na mwekezaji huyo lirejeshwe mikononi mwao, ili waweze kuzalisha mazao yao ya aina mbalimbali.

No comments: