Monday, July 11, 2016

KAMPUNI YA MANTRA TANZANIA YATOA MSAADA WA MADAWATI 500 MKOANI RUVUMA

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Bilinith Mahenge akikagua madawati yaliyotolewa na kampuni ya Mantra Tanzania inayojishughulisha na utafutaji wa madini ya uran katika mto Mkuju wilayani Namtumbo mkoani humo, ikiwa ni lengo la kukabiliana na upungufu wa madawati kwa shule za msingi na sekondari katika mkoa wa Ruvuma upande wa kulia ni mkurugenzi mkuu wa Mantra, Frederick Kibodya.

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Bilinith Mahenge upande wa kulia akipokea moja kati ya madawati 500  kutoka kwa Mkurugenzi mkuu wa kamapuni ya Mantra Tanzania, Frederick Kibodya inayojihusisha na utafutaji wa madini ya Uran katika mto Mkuju wilayani Namtumbo. Mantra imetoa madawati 500 yenye thamani ya shilingi milioni 40  yatakayosaidia kupunguza uhaba wa madawati kwa shule za msingi na sekondari mkoani Ruvuma.

Na Kassian Nyandindi,
Songea.

KAMPUNI ya Mantra Tanzania, imekabidhi  madawati 500 yenye thamani ya shilingi milioni 40 kwa Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge ikiwa ni mwitikio wa agizo la Rais Dkt. John Magufuli kwa wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi, kuchangia utengenezaji wa madawati hayo ili kuweza kukabiliana na upungufu uliopo katika shule za msingi na sekondari hapa nchini.

Msaada huo unafuatia uamuzi wa serikali ya awamu ya tano wa kutoa elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne kwa wanafunzi ambao hapo awali walikuwa wanakosa haki ya kupata elimu, hatua ambayo imechangia ongezeko kubwa la wanafunzi darasani na kusababisha uhaba mkubwa wa madawati.

Mbali na upungufu wa madawati pia imesababisha kuwepo kwa uhaba wa vifaa vya muhimu mashuleni ikiwemo viti, meza, vitabu na baadhi ya vifaa vingine kwa ajili ya matumizi ya wanafunzi hivyo serikali inaendelea kuwaomba wadau hao kutoa michango yao ili kufikia malengo ya  ufumbuzi wa tatizo hili na kwamba serikali ya mkoa wa Ruvuma, iliiomba kampuni ya Mantra Tanzania na wadau wengine wa mkoa huo kuchangia madawati hayo kwa lengo la kuweza kukabiliana na tatizo hilo.


Mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo,  Frederick Kibodya alisema kuwa msaada huo wa madawati umetolewa kwa lengo la kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Rais John Magufuli kwa kutoa elimu bure ya msingi na sekondari hapa nchini, kwa kuongeza pia ubora wa elimu na kuboresha mazingira ya kusomea wanafunzi.

Alisema kampuni ya Mantra inaamini kwamba, madawati hayo yatatoa mchango chanya katika kuleta ari ya kujifunza kwa watoto 1,500 na kuwahamasisha kwenda shule kila siku, kushiriki kikamilifu masomo yao na kuandika mwandiko mzuri tofauti na kukaa chini sakafuni.

Kwa mujibu wa Kibodya ni kwamba, Mantra ina imani kwamba mchango huo wa madawati 500 utachangia pia katika kuboresha kiwango cha elimu mkoani Ruvuma, ambako inaendesha shughuli zake.

Kibodya alieleza kuwa tangu kampuni hiyo ianze utafiti wa madini aina ya Urani katika mradi wake wa Mkuju, wilayani Namtumbo mkoani humo imekuwa na jitihada ya kuendelea kuchangia na kuboresha mazingira ya upatikanaji wa elimu bora kwa kuchangia madawati, vitabu kwa baadhi ya shule za sekondari.

Vilevile wameweza kujenga miundombinu ya umeme wa nishati ya jua, ujenzi wa maabara ya sayansi katika shule hizo ambapo mbali na hayo, Mantra pia imekuwa ikisaidia kuboresha mazingira na sekta ya afya wilayani Namtumbo na Tanzania kwa ujumla.

Kampuni ya Mantra inatekeleza pia mpango wake wa kupambana na ujangili kwa kutambua tembo wa Tanzania ndio miongoni mwa wanaouawa hivyo katika kutekeleza jambo hilo, imechukua hatua kwa kuzindua operesheni kali na ya teknolojia ya juu katika kupambana na ujangili huo kwa kushirikiana na idara ya Wizara ya Maliasili na Utalii.

Aliongeza kuwa kampuni hiyo ambayo inamiliki mradi huo wa Urani katika mto Mkuju wilayani Namtumbo ni kampuni tanzu ya Uranium One na shirika lake kuu la ROSATOM, ambalo ni shirika la nishati ya Atomiki la serikali ya Urusi na kampuni ya Uranium One ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa urani duniani ikiwa na umiliki wa aina mbalimbali katika nchi za Kazakhstan, Marekani, Australia na Tanzania.

No comments: