Monday, July 11, 2016

GAMA: MIKOPO INAYOTOLEWA NA TAASISI ZA KIFEDHA YENYE RIBA KUBWA NI KIKWAZO CHA MAENDELEO YA WANANCHI



Na Julius Konala,
Songea.

MBUNGE wa jimbo la Songea mjini kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Ruvuma, Leonidas Gama amesema kuwa mikopo inayotolewa na taasisi za kifedha kwa riba kubwa, imekuwa ni kikwazo cha maendeleo ya wananchi katika kupambana na umaskini.

Leonidas Gama.
Gama alisema hayo juzi wakati alipokuwa akizungumza na vikundi mbalimbali vya wajasiriamali mjini hapa, ambavyo vinaratibiwa na Jumuiya ya Mabinti wa Maria Immaculata (DMI) mjini Songea.

Alisema kuwa mikopo hiyo imekuwa sio msaada kwa wananchi, badala yake imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa kuwaingiza katika dimbwi la umaskini kutokana na baadhi yao wanaposhindwa kuirejesha, mali zao hunyang’anywa na kuuzwa.


Kufuatia hali hiyo mbunge huyo, amewataka wananchi kujiunga kwenye vikundi mbalimbali vya ujasiriamali ili waweze kupata mikopo inayotolewa na serikali  kwa riba nafuu.

Aidha amevipongeza vikundi vya ujasiriamali vinavyoratibiwa na Jumuiya hiyo ya DMI, kwa kukidhi vigezo vya kukopesheka huku akiwataka pia kutumia mikopo wanayoipata kwa malengo yaliyokusudiwa na sio vinginevyo.

Vilevile ameonya kutumia mikopo hiyo kwa mambo ya anasa na kuongeza nyumba ndogo, badala yake waitumie kwa nidhamu pamoja na kuirejesha kwa wakati.

Akizungumza katika mkutano huo, naye Mratibu wa mifuko ya uwezeshaji toka baraza la taifa la uwezeshaji wananchi kiuchumi, Nyakao Mahemba alifafanua kuwa vikundi hivyo vya DMI vimekidhi vigezo baada kufungua akaunti katika benki ya Posta na kujiwekea akiba.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa vikundi hivyo mkoani Ruvuma, Speciosa Katambala, amemuhakikishia mbunge huyo kuwa yale yote aliyowaagiza watayafanyia kazi ikiwemo kuendelea kuhamasisha wananchi wilaya zote za mkoa huo, kuendelea kujiunga na vikundi hivyo pamoja na kutumia mikopo watakayopata kwa malengo yaliyokusudiwa.

No comments: