Thursday, July 14, 2016

WANANCHI WAIWEKEA MAGOGO BARABARANI KAMATI YA KUCHUNGUZA MGOGORO WA ARDHI MAKETE NJOMBE



Na Kassian Nyandindi,

Njombe.

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida wananchi wa kijiji cha Mbalatse wilayani Makete mkoa wa Njombe, wameweka magogo makubwa barabarani kuzuia Kamati iliyoundwa na uongozi wa wilaya hiyo kwenda kijijini hapo kuchunguza mgogoro wa ardhi uliopo kati ya wananchi wa kijiji hicho na mwekezaji wa Kampuni ya Silverland Tanzania, kwa madai kuwa amepora ardhi yao zaidi ya hekta 3,000 ambazo zilikuwa zikiwasaidia kuzalisha mazao ya aina mbalimbali.   

Wananchi hao ambao walionekana kuwa na jazba walizuia magari yaliyowaleta wajumbe wa kamati hiyo na mwekezaji huyo katika ofisi za makao makuu ya kata hiyo, walionekana kuwa na hasira huku wengine wakiimba nyimbo kwa sauti kubwa wakisema, “tunataka turudishiwe mashamba yetu, aliyotunyang’anya mwekezaji.

William Lukuvi.
Tukio hilo la aina yake lilitokea Julai 14 mwaka huu majira ya mchana kwenye eneo la ofisi za kata ya Mbalatse, ambako umati mkubwa wananchi ulikusanyika kwa lengo la kujua hatma ya mgogoro huo uliopo kati yao na mwekezaji huyo.

Aidha wananchi hao wamemuomba Waziri wa ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi William Lukuvi kuona umuhimu wa kuingilia kati kutatua mgogoro huo ambao unatishia usalama wa maisha yao.

Walisema kuwa kufuatia ardhi hiyo kuchukuliwa na mwekezaji huyo, wananchi hao wanakosa maeneo ya kulima mazao ya chakula na biashara jambo ambalo hivi sasa, baadhi yao wanalazimika kwenda kwenye maeneo karibu na vyanzo vya maji kulima mazao hayo.


Wakihojiwa na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti, wananchi hao walifafanua kuwa miaka iliyopita kwa muda mrefu walikuwa wakilima mahindi kwa wingi katika eneo hilo ambalo ni maarufu kwa jina la Ludodolela, ambalo lina rutuba tofauti na maeneo mengine yaliyopo kwenye kata hiyo.

Aloyce Chaula mkazi wa kijiji cha Mbalatse alifafanua kuwa tangu kuzaliwa kwake miaka ya 60 iliyopita wazazi wake pamoja na wananchi wengine wa kata hiyo walikuwa na mashamba yao katika eneo hilo ambalo amepewa mwekezaji, bila wananchi kushirikishwa hivyo wanaiomba serikali kupitia Wizara hiyo kunusuru hali hiyo ili wananchi wa kata hiyo waweze kurejeshewa mashamba yao.

“Ndugu waandishi wa habari mnaliona kundi hili kubwa la wananchi wakilalamikia kuporwa maeneo yao, kwani awali huyu mwekezaji alikuja hapa kwetu kijijini kuomba eneo dogo kwa muda kwa ajili ya kufanya majaribio ya kupanda mbegu za zao la shairi, lakini tuna mshangaa ghafla amemilikishwa eneo kubwa na sisi wazawa tumefukuzwa huku akiendelea na uzalishaji wa zao hili la shairi”, alisema Chaula.

Kwa upande wake Damian Mwinuka mkazi wa kijiji hicho alieleza kuwa kufuatia mwekezaji huyo kunyang’anya eneo hilo la mashamba bila kufuata taratibu za utwaaji ardhi, hivi sasa vijana wengi wanakwenda mikoa ya jirani kwenda kutafuta mashamba ya kulima wakati nyumbani kwao kulikuwa na eneo kubwa la kuweza kuzalisha mazao mbalimbali ikiwemo viazi mviringo, ufuta, alizeti na ngano.

Alisema kuwa kutokana na usumbufu huo wanaoupata sasa, bado wanalazimika kuiangukia serikali ili iweze kuwasaidia na ardhi yao irejeshwe mikononi mwao na sio vinginevyo.

Uchunguzi uliofanywa na waandishi wa habari umebaini pia katika mashamba hayo yanayolalamikiwa, mwekezaji huyo wa Silverlands Tanzania yenye makao makuu yake Ifunda mkoani Iringa ndiyo inayoendesha shughuli za kilimo cha zao la shairi kwenye eneo hilo linalolalamikiwa na wananchi hao.

Waandishi hao wamezungumza na Meneja wa Kampuni hiyo Steven Maina alisema kuwa ndani ya eneo hilo, wao wana hati miliki na kwamba kuna kiwanja cha ndege ambacho kimekuwa kikitumika ndege kutua kipindi cha kiangazi, wakati wa mavuno ya zao hilo na kwamba pia kumejengwa majengo ya ofisi na nyumba za kuishi wafanyakazi wa shamba hilo.

Maina alifafanua kuwa sehemu ya shamba hilo kumezalishwa kwa wingi zao la shairi alizeti, ngano na mboga mboga pamoja na miti ya asili na kwamba haoni sababu ya mgogoro huo kuendelezwa huku akishauri kwamba kuna kila sababu ya serikali kuchukua hatua ya kumaliza tofauti zilizopo.

Naye diwani wa kata ya Mbalatse, Edson Msigwa alisema kuwa malalamiko hayo ya wananchi ni ya kweli kwa kile alichodai kuwa mwekezaji huyo alipewa ekari 70 tu kwa muda kwa lengo afanye majaribio ya kupanda mbegu za zao la shairi, lakini wanashangaa kuona amezalisha ekari zaidi ya 3,000 na kujimilikisha maeneo hayo bila wananchi kushirikishwa.

Msigwa alisema kuwa kufuatia kuwepo kwa mkanganyiko huo, tayari hatua zimechukuliwa kwa kwenda halmashauri ya wilaya ya Makete kuutaka uongozi husika kuona namna ya kumaliza tatizo hilo, kabla machafuko hayajatokea kama ilivyo kwa maeneo mengine ya nje ya mkoa wa Njombe.

“Wananchi wa kata yangu wapo tayari kufunga safari kwenda kuonana na Waziri mwenye dhamana, ili waweze kupata haki zao za msingi juu ya madai haya ya ardhi yao kutokana na hivi sasa wanakosa maeneo ya kuzalisha chakula”, alisema Msigwa.

Pia baada ya diwani huyo kuingilia kati na kutuliza hasira za wananchi hao, ndipo walichukua hatua ya kuyaondoa magogo makubwa waliyokuwa wameyaweka barabarani kwa lengo la kuzuia magari ya wajumbe wa kamati hiyo na mwekezaji yaweze kuondoka, mara baada ya kamati hiyo kukamilisha taratibu zake.

Hata hivyo Kaimu Mkuu wa wilaya ya Makete, Merina Ijiko ambaye pia ni afisa tawala wa wilaya hiyo alipohojiwa alisema kuwa kitendo walichofanya wananchi hao cha kuzuia magari hayo ni kosa, kwa kuwa Kamati hiyo imeundwa kisheria kwa ajili ya kuchunguza mgogoro huo kati yao na mwekezaji huyo hivyo amewataka kupunguza jazba wakati tatizo hilo linafanyiwa kazi.

No comments: