Monday, July 4, 2016

UJENZI WA STENDI KUU YA MAGARI YA ABIRIA SONGEA WAINGIA DOSARI



Na Kassian Nyandindi,
Songea.

UJENZI wa stendi kuu ya magari ya abiria Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, umeingia dosari kufuatia Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) tawi la Songea mkoani humo, kuinyoshea kidole Halmashauri ya Manispaa hiyo kutokana na kujenga uzio kwenye eneo hilo ambalo wanatambua kuwa ni sehemu ya makazi ya watu wakifanyia biashara zao za aina mbalimbali.

Aidha walisema kuwa wameshangazwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa hiyo kupuuza ombi la kumtaka asitishe ujenzi wa uzio huo wa tofari zilizotengenezwa kwa a saruji mpaka atakapokaa na wafanyabiashara hao, ili waweze kuona namna gani ujenzi unafanyika ili kuweza kuondoa malalamiko yasiyokuwa ya lazima.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida Julai Mosi mwaka huu majira ya mchana, baadhi ya wanajumuiya ya wafanyabiashara hao Songea mjini walikusanyika na kwenda katika eneo hilo la stendi kuu, kupinga ujenzi huo usifanyike mpaka kero zao zitakaposikilizwa na viongozi wa halmashauri hiyo.

Tukio hilo ambalo lilishuhudiwa na waandishi wa habari, Nico Challe ambaye ni Katibu wa wafanyabiashara hao alisema wameamua kufanya hivyo baada ya kuona viongozi wa Manispaa hiyo, wamekuwa wakijichukulia maamuzi peke yao bila kushirikisha wadau husika.


“Malalamiko na mombi ya wafanyabiashara katika kituo hiki cha mabasi yaliandikwa kwa barua tangu Mei 30 mwaka huu, kwenda kwa Mkurugenzi wa halmashauri hii tukimtaka asitishe ujenzi mpaka tutakapokaa pamoja na kushauriana namna ya kufanya, lakini cha kushangaza tumepuuzwa hakuna majibu yoyote tuliyopewa na ujenzi kama hivi unaendelea”, alisema Challe.

Naye January Ndumbaro ambaye naye pia ni mfanyabiashara katika eneo hilo, alifafanua kuwa ujenzi huo umesababisha kuharibu hata miundombinu ya maji ya bomba na kusababisha bomba hilo linalopeleka maji kwa wakazi wa mtaa wa Mfanyaranyaki mjini hapa, kukosa huduma kutokana na miundombinu husika kuharibiwa.

Aliongeza kuwa hata vibanda vyao ambavyo wamevijenga ndani ya eneo hilo la biashara wameambiwa wavibomoe kwa madai kwamba wanapaswa kupisha, ili katika eneo hilo lililopo na vibanda hivyo liweze kujengwa kibanda cha kupumzikia abiria huku mkataba wake, akiwa kama mpangaji ukionesha muda wake bado haujaisha.

Kadhalika mfanyabiashara aliyejitambulisha kwa jina la Sabina Mkalanga aliongeza kuwa kuna kila sababu kwa mamlaka husika, kuona umuhimu wa namna ya kumaliza kero hiyo iliyojitokeza na sio kulazimisha kwa matakwa yao binafsi bila kushirikisha jamii.

Ujenzi wa uzio huo katika eneo la stendi kuu ya mabasi ya abiria Songea mjini, unafanywa na mkandarasi ambaye amewekwa na Halmashauri hiyo ambapo hata kibao kinachoelekeza ujenzi huo hakijawekwa na kwamba wakati wafanyabiashara hao wanaingia katika eneo la stendi hiyo kupinga ujenzi wa uzio usiendelee kufanyika, mtu mmoja ambaye hakutaka kujitambulisha jina lake akidaiwa kuwa ndiye msimamizi mkuu anayesimamia ujenzi huo alikimbia na kutokomea kusikojulikana baada ya kuona kundi hilo la watu likielekea katika eneo la ujenzi unapofanyika.

Alipoulizwa Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Manispaa ya Songea, Jenifer Homoro alithibitisha kuwepo kwa malalamiko hayo na kuwataka waandishi wa habari kwenda kumuona Mhandisi wa ujenzi wa Manispaa hiyo, Godfery Majuto ili aweze kutolea ufafanuzi juu ya kero hiyo.

Hata hivyo Majuto alipohojiwa alisema kuwa uzio huo unajengwa baada ya Madiwani wa halmashauri hiyo, kuketi kupitia vikao husika na kukubaliana ujenzi ufanyike ili kuweza kuzuia watu kuingia hovyo na halmashauri kukusanya mapato yake kwa ufanisi mzuri.

No comments: