Saturday, July 2, 2016

MBINGA WAJIVUNIA KUKAMILISHA ZOEZI LA UTENGENEZAJI WA MADAWATI


Madawati ya shule ya msingi ambayo yametengenezwa wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma yakisubiri kuunganishwa, katika karakana mojawapo iliyopo mjini hapa na baadaye kusambazwa mashuleni baada ya kukamilika utengenezaji wake.  

Baadhi ya mafundi wakipandisha madawati kwenye gari kwa ajili  kusambaza katika shule mbalimbali za msingi na sekondari wiayani humo, ambapo wilaya ya Mbinga kupitia halmashauri zake mbili ya mji na wilaya zimefanikiwa kumaliza  tatizo la uhaba wa madawati kwa shule hizo.


Na Muhidin Amri,
Mbinga.

WILAYA ya Mbinga mkoani Ruvuma, kupitia halmashauri zake mbili  ya mji wa Mbinga na wilaya hiyo, imefanikiwa kukamilisha mradi wa utengenezaji madawati kwa ajili ya kukabiliana na tatizo la upungufu uliopo katika shule za msingi na sekondari wilayani humo.

Kazi hiyo imefuatia utekelezaji wa agizo la Rais Dkt. John Magufuli kwa Wakurugenzi, Wakuu wa wilaya na mikoa hapa nchini kuhakikisha kwamba wanatumia rasimali za misitu iliyopo katika maeneo yao, ili kumaliza tatizo hilo la uhaba wa madawati na kuwafanya watoto waliopo shuleni kushindwa kufanya vizuri katika masomo yao kutokana na kukosa madawati ya kukalia wanapokuwa darasani.

Mkurugenzi mtendaji wa Hamashauri ya wilaya ya Mbinga, Venance Mwamengo alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu ambapo alifafanua kwamba wilaya hiyo, ilikuwa na upungufu wa madawati 12,952 kati ya hayo kwa shule za msingi ni 8,452 na kwa shule za sekondari upungufu wa viti na meza ulikuwa 4,500.


Alifafanua kuwa hadi kufikia Juni 30 mwaka huu ambao ni muda wa mwisho wa utekelezaji wa agizo hilo, tayari Halmashauri yake ilifanikiwa kutengeneza madawati 8,000 hivyo kubakia madawati 4,50 ambayo  wanatarajia kukamilisha ndani ya siku chache zijazo kutokana na vifaa vyote muhimu  kama vile nondo na mbao vipo tayari kwa ajili ya kukamilisha kazi hiyo.

Pia Mwamengo alisema kwa shule za sekondari  wamekamilisha kazi hiyo na kubakiwa na ziada ya viti na meza  1,000 ambazo  zitasambazwa katika shule za msingi, zinazokabiliwa na  upungufu huo kwa lengo la kumaliza kabisa tatizo hilo la madawati katika wilaya hiyo.

“Hapa tayari tumefanikisha kumaliza kazi ya kutengeneza viti na meza kwa shule za sekondari na sasa tunaendelea kumalizia kuunganisha madawati yaliyobakia kwa shule za msingi ambapo ndani ya siku chache, tutakuwa tumeshamaliza zoezi hili”, alisema.

Kwa mujibu wa Mwamengo ni kwamba wilaya ya Mbinga, ilitenga  kiasi cha shillingi milioni 475,820 kwa ajili ya  kukabiliana na upungufu wa madawati, meza na viti  kwa shule za msingi na sekondari.

Alifafanua kuwa kiasi hicho cha fedha ni gharama za kununulia mashine za kuranda, kukata na kukunja vyuma, mashine za kupasulia mbao, umeme na gharama zingine ndogo ndogo ambapo vyote kwa ujumla vimetengenezwa kwa kutumia mbao pamoja na chuma ili kufanya viweze kuwa imara zaidi, ikilinganishwa na madawati yanayotengenezwa kwa mbao tupu ambayo huharibika haraka.

No comments: