Sunday, July 31, 2016

KAMPUNI YA TUTUNZE YAPONGEZWA KUCHANGIA SHUGHULI ZA MAENDELEO YA WANANCHI

Ofisi za makao makuu ya Kampuni ya Tutunze Kahawa Limited (TKL) zilizopo Mbinga mjini.


Na Kassian Nyandindi,      
Mbinga.

WADAU wa maendeleo wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma wameipongeza Kampuni ya Tutunze Kahawa Limited (TKL) iliyopo wilayani hapa, kwa jitihada zake za kuunga mkono na kuchangia shughuli mbalimbali za maendeleo ya wananchi wilayani humo.

Pongezi hizo zilitolewa juzi mjini hapa, wakati kampuni hiyo ilipokuwa ikikabidhi madawati 20 yenye thamani ya shilingi milioni 1.9 kwa uongozi wa halmashauri ya wilaya hiyo kwa ajili ya kukalia wanafunzi shuleni.

Walisema kuwa juhudi hizo zinazofanywa na TKL kuna kila sababu kwa makampuni mengine yaliyopo wilayani Mbinga, kuiga mfano huo katika kuchangia michango ya maendeleo ili wilaya hiyo iweze kusonga mbele na kukua kiuchumi.

Aidha naye Meneja masoko wa kampuni hiyo, Thomas Ngapomba kwa upande wake alisema kuwa katika juhudi za kuunga mkono kampeni iliyoanzishwa na Rais Dkt. John Magufuli ya kuondoa tatizo la madawati kwa shule za msingi na sekondari hapa nchini, Tutunze Kahawa Limited nayo iliona kuna umuhimu wa kuchukua jukumu la kuchangia madawati hayo kwa wilaya ya Nyasa na Mbinga.

Ngapomba alifafanua kuwa lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha kwamba wanafunzi wanakuwa na mazingira mazuri ya kusomea, pale wanapokuwa darasani ili waweze kuandika mwandiko mzuri.


Alisema kuwa tokea kampuni hiyo ianzishwe mwaka 2009 wilayani humo na kujishughulisha na biashara ya zao la kahawa, imeweza kutoa michango yenye thamani ya shilling milioni 34.9 katika sekta ya elimu, afya na jamii kwa ujumla.

Vilevile alibainisha kuwa shule ya Makita sekondari iliyopo Mbinga mjini ilikabidhiwa msaada wa kompyuta tano na vifaa vya kufundishia tekinolojia ya mawasiliano, huku shule ya Lusetu sekondari iliyopo katika kata ya Luwaita, jengo la shule hiyo lenye vyumba viwili vya maabara vilifanyiwa ukarabati.

“Mifuko 250 ya saruji, ukarabati wa maabara kwenye shule za sekondari wilayani Mbinga tumekuwa tukiufanya na pia shule ya sekondari Kikolo iliyopo kata ya Kikolo wilayani hapa, tumetoa mchango wa mifuko 40 ya saruji kwa ajili ya kukarabati vyumba vya madarasa”, alisema Ngapomba.

Kadhalika alisema kuwa Maguu sekondari iliyopo kata ya Maguu, Dkt. Shein sekondari kata ya Mpepai walipewa mchango wa mifuko 50 ya saruji kwa kila shule, Mikiga sekondari Mbinga mjini ilipewa mabati 100 na mifuko 30 ya saruji kwa ajili ya kukamilisha ukarabati vyumba vya madarasa na kwamba wamekarabati pia mfumo wa kuleta maji safi, kwenye kijiji cha Myangayanga kwa kukarabati mabomba na viunganishi vyake.

“Tumeshiriki pia kikamilifu katika kuboresha mazingira kwa kufanya usafi katika mji wa Mbinga, tumefunga vifaa vya nguvu ya sola kwenye zahanati ya kijiji cha Nyoni kata ya Nyoni”, alisema.
  
Kwa wilaya ya Nyasa katika kipindi cha mwaka huu, kampuni hiyo ya Tutunze Kahawa Limited imechangia kwa kutoa vifaa vya kufanyia ukarabati nyumba ya mganga zahanati ya kijiji cha Kingirikiti kata ya Kingirikiti wilayani humo, vyenye thamani ya shilingi milioni 8,000,000 pamoja na mchango wa madawati 20 ya kukalia wanafunzi darasani yenye thamani ya shilingi milioni 1.9.

No comments: