Wednesday, July 27, 2016

NYASA WATAKA UJENZI WA VITUO VYA MAFUTA



Na Kassian Nyandindi,         
Nyasa.

BAADHI ya wananchi wa wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, wamesema kwamba wanapata adha kubwa na hufikia hatua ya kushindwa kufanya shughuli zao mbalimbali za kimaendeleo, kutokana na ukosefu wa huduma ya vituo vya kuuza mafuta katika wilaya hiyo.

Aidha wameomba watu wenye uwezo mkubwa wa kifedha, kujitokeza kwenda wilayani humo kuwekeza katika sekta hiyo muhimu hatua ambayo itarahisisha upatikanaji wa huduma hiyo na kuharakisha kukua kwa shughuli zao za kiuchumi.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi wenzake, mkazi mmoja wa mji wa Mbamba bay wilayani Nyasa Petro Ndembele alisema kuwa wilaya hiyo tangu ianzishwe mwaka 2013 hakuna huduma ya vituo vya kuuza mafuta, jambo ambalo linachangia kwa kiasi kikubwa maisha ya wakazi wengi wilayani hapa kuwa magumu sambamba na kuongezeka kwa nauli kutoka sehemu moja kwenda nyingine katika magari ya kusafiria abiria na kuwafanya waendelee kuwa maskini.


Ndembele alisema kuwa ukosefu huo wa mafuta husababisha kushindwa kuwaokoa hata ndugu zao, pale yanapotokea maafa ndani ya Ziwa Nyasa kwani hushindwa kuwafikia kwa haraka  kwa kutumia boti, maeneo ya ajali inapotokea na kulazimika kutumia muda mrefu kuwatafuta ndugu na jamaa zao ambao hupoteza maisha katika ziwa hilo.

Kwa mujibu wa Ndembele alisema endapo kungekuwepo vituo maalumu vya kuuzia mafuta badala ya utaratibu unaotumika sasa, ambapo wafanyabiashara wachache kutoka wilaya jirani ya Mbinga wanakwenda kufanyabiashara hiyo kwa kutumia maguduria na ndoo, ambavyo vinachangia kupunguza ubora wa mafuta hayo kutokana na baadhi yao kuwa na tabia ya kuyachakachua.

Pia amepongeza juhudi kubwa za serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli ya kupambana na vitendo vya wizi, ufisadi na uzembe kwa watumishi wa umma hasa kwa wale waliozoea kufanya kazi kwa mazoe huku wakijifanya wao ni miungu watu, kwani hatua hiyo itasaidia kuharakisha upatikanaji wa huduma za kijamii na suala zima la kukuza maendeleo katika maeneo mbalimbali hapa nchini.  

Alisema kuwa hata kukosekana kwa huduma  za kijamii kwa baadhi ya maeneo hapa nchini, kumechangiwa na watumishi ambao walifanya kazi kwa ajili ya kujinufaisha matumbo yao, kwani fedha ambazo walizitumia kwa ajili ya  maslahi yao binafsi zingewezesha kupeleka huduma husika kwa wananchi hasa  wa maeneo ya vijijini.

Kwa upande wa suala la uhaba wa madawati kwa shule za msingi na sekondari hapa nchini, Ndembele alisema tatizo hilo limesababishwa na uzembe  uliofanywa na baadhi ya watumishi waliopewa dhamana ya kusimamia rasilimali za nchi na kuzitumia vibaya, huku wakiacha kwa makusudi kutatua shida na kero za Watanzania wengine ambapo amemuomba Rais Magufuli kuendelea kuwatumbua watumishi hao ambao wanaifilisi nchi yetu.

Hata hivyo amewataka wananchi kutumia muda wao kufanya kazi za kujiletea maendeleo, badala ya kutumia muda mwingi kufanya anasa kwa sababu jambo hilo limekuwa likichangia umaskini licha ya Tanzania kubahatika kuwa na rasilimali nyingi ambazo hadi sasa bado hazijatumika kikamilifu kwa ajili ya kujipatia maendeleo.

No comments: