Wednesday, July 20, 2016

SERIKALI KUJENGA VYUO VYA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI KWA AJILI YA KUSOGEZA HUDUMA HUSIKA KWA WANANCHI

Naibu  Waziri wa Elimu Sayansi  na Teknolojia, Mhandisi Stella Manyanya akiangalia ramani ya kiwanja cha ujenzi wa chuo cha VETA wilayani Namtumbo mkoa wa Ruvuma. (Picha na Moses Konala)

Na Yeremias Ngerangera,
Namtumbo.

IMEELEZWA kuwa serikali hapa nchini, katika mwaka huu wa fedha inatarajia kujenga vyuo vya Elimu na Mafunzo ya Ufundi stadi (VETA) katika wilaya ya Njombe, Ludewa, Geita  na  Namtumbo  ikiwa ni lengo la kuwasogezea wananchi huduma husika kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Aidha katika wilaya hizo ambako ujenzi huo utafanyika, viongozi waliopewa dhamana ya kusimamia suala hilo wametakiwa kujenga ushirikiano na kuhakikisha kwamba, ujenzi huo unakamilika kwa wakati ili kuweza kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Stella Manyanya  alisema hayo juzi alipokuwa kwenye ziara yake ya kikazi wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma, kukagua eneo ambalo linatarajiwa kujengwa chuo hicho wilayani humo.


“Nimeridhishwa na ukubwa  wa eneo hili lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa  chuo  hiki cha VETA hapa Namtumbo, natoa agizo kwa viongozi wote wa wilaya ambako ujenzi huu utafanyika kusimamia kikamilifu zoezi hili ili serikali iweze kufikia malengo yake ya maendeleo tuliyojiwekea kwa wananchi wetu”, alisisitiza Manyanya.

Manyanya alimtaka pia Mkuu wa wilaya hiyo, Luckness Amlima kushirikiana na wataalamu watakaopewa dhamana ya ujenzi wa chuo hicho kwa kuwa wabunifu na kuelimisha jamii juu ya elimu itakayotolewa chuoni hapo mara ujenzi utakapokamilika, itaendana na nyakati za viwanda na sio vinginevyo.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Namtumbo, Amlima alimhakikishia Naibu Waziri huyo kwamba mara ujenzi huo utakapoanza atausimamia kwa umakini mkubwa, ili adhma hiyo ya serikali iweze kufikia malengo yake.

Pamoja na mambo mengine, akitoa taarifa ya maendeleo ya eneo linapojengwa chuo hicho cha mafunzo ya ufundi stadi, Afisa ardhi na maliasili Maurus Hyera  alifafanua kuwa eneo lililotengwa lina ekari 30 ambalo tayari limepimwa kwa ajili ya kuanza ujenzi huo.

No comments: