Wednesday, July 27, 2016

MADIWANI CUF TUNDURU WAHAMASISHA UJENZI WA MADARASA

MKUU wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Juma Homera upande wa kushoto akishiriki kwa vitendo katika zoezi la kufyatua tofari za shule ya Msingi Umoja iliyopo kata ya Nanjoka wilayani humo, Kushoto kwake ni Mratibu Elimu Kata Issa Selemani na wa mwisho kushoto ni diwani wa kata hiyo, Rajab Mkwawa ‘Mtimbalugono’.


Na Steven Augustino,
Tunduru.

MADIWANI wa Chama Cha Wananchi (CUF) wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wameahidi kuunga mkono kwa vitendo juhudi zinazofanywa na serikali ya awamu ya tano, katika kuondoa kero mbalimbali zinazowakabili wananchi wa wilaya hiyo ili waweze kusonga mbele kimaendeleo.

Ahadi hiyo ilitolewa na Madiwani wa kata ya Nanjoka, inayoongozwa na Rajab Mtimbalugono, kata ya Majengo, Abdallah Rajabu na diwani wa kata ya Mlingoti Mashariki, Mohamed Aloyce. 

Madiwani hao walisema hayo walipokuwa wakizungumza na Mkuu wa wilaya ya Tunduru, Juma Homera alipowatembelea katika eneo la kufyatulia matofari kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ya shule ya msingi Umoja iliyopo mjini hapa.


Diwani wa kata ya Nanjoka, Rajab Mkwawa alisema kuwa maamuzi hayo wamefikia baada ya kubaini uwepo wa pungufu mkubwa wa miundombinu ya kufundishia katika shule zilizopo katika maeneo yao na kwamba wamepanga kufyatua tofari 60,000 ili kukidhi mahitaji ya ujenzi wa madarasa hayo.

Alisema kuwa baada ya kutambua tatizo hilo la upungufu wa madarasa, wamefanya uhamasishaji kwa wananchi kuchangia nguvu zao, katika shule zilizopo katika maeneo yao.

Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Umoja wilayani humo, Amina Kachepa alifafanua kuwa shule hiyo ina wanafunzi 557 ambapo ina upungufu wa vyumba vya madarasa sita, ofisi mbili, nyumba saba za kuishi walimu, vyoo matundu 12 na madawati 162.

Akitolea ufafanuzi wa taarifa hiyo, Kachepa alimweleza Mkuu wa wilaya ya Tunduru, Homera kuwa wanafunzi hao wamekuwa wakisoma chini ya miti nyakati za kiangazi kutokana na upungufu wa madarasa na kwamba nyakati za masika wamekuwa wakisoma kwa mtindo wa kupokezana katika vyumba hivyo vya madarasa vilivyopo sasa.

Akijibu kero hizo Mkuu wa wilaya ya Tunduru, Homera pamoja na kupongeza jitihada hizo zinazofanywa juu ya ujenzi wa madarasa hayo alisema serikali nayo itaendelea kuunga mkono jitihada hizo, kwa kununua vifaa vya kiwandani ili ujenzi uweze kukamilika kwa wakati pale utakapoanza kufanyika.

Homera alisema kuwa kitendo cha viongozi na wananchi hao kuonesha moyo wa kujitoa na kujitolea katika kazi hiyo, wanatakiwa kuhakikishiwa usalama wa maisha na mazingira bora ya kufundishia.

No comments: