Tuesday, July 19, 2016

MAKALA YA UCHUMI: USHIRIKA NYASA NA MIKAKATI YA KUMKOMBOA MKULIMA


Hii ni moja kati ya mashine ya kisasa ya kukobolea kahawa mbivu iliyofungwa katika chama cha ushirika Luhangarasi wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, ambayo hukoboa kahawa kwa viwango bora vinavyokubalika ambapo wakulima wa zao hilo husisitizwa kukoboa kahawa kwa kutumia mashine kama hiyo ili iweze kuwa katika ubora. (Picha na Kassian Nyandindi)


Na Kassian Nyandindi,

KINYWAJI kama kahawa ni moja kati ya bidhaa muhimu na maarufu inayopendwa duniani, vilevile ni chanzo cha mapato kwa nchi zinazohusika na soko hilo, ambapo uzalishaji wa zao hili si kazi rahisi bali ni kazi ngumu inayohitaji ujuzi wa hali ya juu.

Aidha katika kuwawezesha wakulima wa zao hilo, kuzalisha kahawa kwa viwango vyenye ubora mara zote sekta husika wakiwemo maafisa kilimo na ushirika ndiyo tunatambua wamepewa jukumu la kuwaelimisha wakulima hao, mara kwa mara namna ya uzalishaji huo.

Wilaya ya Nyasa iliyopo mkoani Ruvuma, ni moja kati ya wilaya ambayo wakulima wake wanazalisha kahawa ambapo jitihada mbalimbali zimekuwa zikifanywa ili kuboresha uzalishaji wake, kwa kuwahimiza wakulima wazingatie kanuni bora za kilimo cha zao hilo.

Katika kuhamasisha wakulima kujiunga kwenye vikundi au ushirika, serikali siku zote imekuwa ikisisitiza jambo hili ikiwemo uzalishaji wa mazao mbalimbali kwa pamoja ili kuongeza ufanisi na muungano huo, ni rahisi wataalamu wa kilimo kuwafikia na kuwapa utaalamu husika kuliko kumpitia mkulima mmoja mmoja.

Siku zote ili kuweza kuzalisha kahawa yenye ubora wakulima  wa zao hilo wilayani humo, wamejiwekea mikakati ya kuendelea kuhamasishana na kujiunga kwenye vyama vya ushirika vya mazao ya chakula na biashara.

Akihutubia katika mkutano mkuu wa ufunguzi wa msimu wa ushirika kwa wanachama wa chama cha ushirika Luhangarasi kilichopo katika kata ya Luhangarasi wilayani Nyasa, Afisa ushirika wa wilaya hiyo Menance Ndomba anawataka wakulima wote wa mazao hayo ya chakula na biashara wajenge dhamira kuu ya kujiunga pamoja ili waweze kuondokana na changamoto ya kufanya biashara na makampuni binafsi, ambayo yamekuwa yakimnyonya mkulima na kumwacha aendelee kubaki kuwa maskini.

Ndomba anasema kuwa wilaya hiyo ina vyama vya ushirika vitano ambavyo ni Mapendo, Lipo, Kingirikiti, Nambawala pamoja na Luhangarasi ambapo wakulima wanaounda ushirika kwenye vyama hivyo wameamua kujiunga kwa umoja wao na kufungua msimu wa ukusanyaji wa kahawa bora, hatimaye kutafuta soko zuri mnadani litakaloweza kuwafanya wauze kahawa yao na kupata faida kwa kila mkulima atakayeuza kahawa yake huko.


Wanachama hao wa vyama hivyo vya ushirika walikutana Juni 11 mwaka huu katika kijiji cha Kimbango kata ya Luhangarasi wilayani hapa, kwa lengo pia la kufungua mtambo wa kukobolea kahawa mbivu ya maganda ambayo humenywa maganda yake, huoshwa na maji safi kisha kuanikwa kwenye vichanja hatimaye kuwa katika viwango vinavyokubalika ili iweze kupata bei nzuri katika soko la dunia.

“Ndugu zangu wakulima nasisitiza pelekeni kahawa zenu kwenye vyama vya ushirika tuache kuuza kwa mtindo wa magoma kwa kubadilishana na bidhaa fulani, tukifanya hivi hakika hatutaweza kunufaika na ushirika wetu”, alisisitiza Ndomba.

Anasema kuwa siku zote wanunuzi binafsi wamekuwa na mbinu za ujanja ambazo hudhoofisha maendeleo ya mkulima na kumwacha aendelee kubaki kuwa maskini, hivyo wanapaswa kulitambua hilo na kukataa kuendelea kukandamizwa na mtu yeyote kwani ushirika ni mahali salama ambapo pana mkono wa serikali ambao humfanya mkulima kuwa salama na mali zake.

Vilevile aliwataka viongozi waliopo katika ushirika huo kuwa waadilifu na mali za wanachama na kuwaelimisha wakulima wapeleke kahawa zao, katika mitambo ya kuchakata kahawa mbivu ili iweze kuwa katika ubora na kupata soko zuri.

Ofisa ushirika huyo wa wilaya ya Nyasa, Ndomba anabainisha kuwa kupitia vyama vya ushirika mkulima amekuwa akinufaika kwa kupata huduma kubwa za aina tatu ikiwemo mafunzo mbalimbali juu ya uendeshaji wa vyama hivyo, kuwaunganisha na masoko ya nje, vyombo vya fedha pamoja na wagavi wa pembejeo bora za kilimo.

Anaeleza kwamba mpango wa mafunzo husaidia kuboresha zao la kahawa kutoka madaraja ya chini ya 10 hadi kufikia daraja la 4 ambapo haya yote, hutokana na matokeo ya matumizi ya kusimika mashine za kati za kisasa ambazo hukoboa kahawa mbivu kwa viwango vinavyokubalika.

Anafafanua zaidi kuwa mashine nyingi hutumia teknolojia ya kisasa ambayo hutumia maji kidogo na kwamba, huondoa sukari kwenye punje ya kahawa wakati wa kukoboa hivyo kutohitaji uvundikaji ambao hupunguza ubora wake.

Anasema ujenzi wa vituo kwa ajili ya kufunga mashine hizi kwenye vikundi unatekelezwa kwa mpango wa ushirikishwaji wa wakulima wenyewe ambapo huchangishana fedha za kuinunua na kujengea banda la mashine, kuleta maji safi kituoni, kujenga visima na mifereji, meza za kuanikia na ghala la kuhifadhia kahawa.

Kuhusu mafunzo ya njia bora za kilimo cha kahawa kwa vikundi husika vilivyosajiliwa kisheria, maafisa kilimo kwa kushirikiana na Taasisi ya utafiti wa zao la kahawa (TACRI) wamekuwa bega kwa bega  katika kufanikisha azma hiyo.

“Pia wataalamu wa kilimo wamekuwa wakipitia taratibu za uanzishwaji wa mashamba darasa kwa kila kikundi na kuweka ushindani kati yao, ikiwa ni lengo la kuhamasisha waweze kuzalisha kahawa iliyobora na ambayo itapata soko zuri”, anasema.

Kwa upande wake Katibu wa vyama vya ushirika wilaya ya Nyasa, Batazary Hyera anaeleza kuwa ndani ya vyama hivyo vitano vya ushirika vilivyopo wilayani humo wameweza kuanzisha pia vyama vya akiba na mikopo (SACCOS) ambavyo vimesajiliwa kwa mujibu wa sheria ya ushirika wa vyama vya akiba na mikopo.

Anasema kwamba vyama hivyo, vimekuwa vikihudumia wanachama wake ambao wenye hisa na wakulima wanaofikia idadi ya 8,663 kila mwaka katika kanda zinazolima mazao ya chakula na biashara.

Hyera anaongeza kuwa wamekuwa wakitoa huduma nyingi za pembejeo za kilimo, ikiwa ni lengo la kukuza na kuboresha mazao ya wakulima hususani kwa kilimo cha zao la kahawa na mahindi katika kanda zinazoshughulika na mazao hayo.

Katika msimu wa mwaka 2015/2016 anasema jumla ya mifuko 7,131 ya pembejeo za kilimo, wameweza kuwakopesha wanachama wao ili kuweza kuongeza uzalishaji na kukuza kipato miongoni mwao.

Pia katika msimu huo walianzisha mfuko wa pembejeo unaomilikiwa na vyama vyenyewe wilayani humo, wenye thamani ya shilingi milioni 33,685,450 ukiwa na malengo ya kupunguza mikopo ya pembejeo ili kumfanya mkulima aweze kumudu gharama zake na kuboresha mazao shambani.

Akizungumzia mikakati waliyojiwekea ya ukusanyaji kahawa Katibu huyo wa vyama vya ushirika wilayani hapa, Hyera anasema kuwa wamejiwekea mikakati ya kukusanya kilo 808,450 za kahawa kwa msimu wa 2016/2017 sawa na ongezeko la asilimia 20 ya makusanyo yaliyokusanywa na vyama hivyo, katika msimu wa mwaka 2015/2016 ambapo yalikuwa kilo 673,709.

Sambamba na hilo, Hyera anaeleza kwamba katika kuboresha ubora wa kahawa vyama hivyo vitano vya ushirika wilayani Nyasa, vitasambaziwa pembejeo za kilimo yaani mbolea mifuko 10,000 katika msimu wa kuelekea kipindi cha mvua 2016/2017 ili wakulima wake, waweze kuboresha mazao yao shambani.

Anaeleza kuwa vyama hivyo pia hivi sasa vinamiliki na kuendesha mitambo 17 ya kuchakata kahawa mbivu, ambayo inaendelea kusimamiwa vizuri na kufanikisha uzalishaji toka tani 249 msimu wa mwaka 2014/2015 hadi tani 673 kwa mwaka 2015/2016.

Hyera anaongeza kuwa siku zote kwenye mafanikio hapakosi changamoto, hivyo wanakabiliwa na tatizo la uwezo mdogo wa vyama kukabili ushindani katika mfumo wa soko huria, kutokana na kuwa na mtaji mdogo wa kuweza kuendeshea vyama hivyo.

Anasema changamoto kubwa nyingine inayowakabili ni uelewa mdogo wa baadhi ya wakulima juu ya uzalishaji bora wa kahawa ambapo baadhi yao wamekuwa na tabia ya kukoboa kahawa zao nyumbani, badala ya kupeleka kwenye mitambo ya kisasa ya kukobolea zao hilo ambayo inamilikiwa na vyama vya ushirika.

Pamoja na mambo mengine anasema, kuanzishwa kwa SACCOS katika ushirika wao kutawawezesha wakulima kuepukana na wafanyabiashara walanguzi ambao huzunguka vijijini na kuwarubuni wakulima, wakope fedha na mwisho wa siku hutakiwa kulipa kahawa wakati wa mavuno.

Hata hivyo anatoa msisitizo kwamba wakati umefika kwa wakulima wenzake kuachana na wafanyabiashara hao wajanja badala yake wajiunge na vyama vya ushirika wilaya ya Nyasa, ili waweze kufaidika pia na mafunzo yanayotolewa kuhusiana na suala zima la uzalishaji wa kahawa bora hatimaye wazalishe kwa wingi na yenye ubora unaokubalika katika soko la kimataifa.

Mwandishi wa makala haya ni mchambuzi pia wa makala za uchunguzi na habari za aina mbalimbali anapatikana kwa simu namba 0762 578960 au barua pepe; nyandindi2006@yahoo.com

No comments: