Tuesday, July 12, 2016

WAZIRI MKUU AWATAKA WAKURUGENZI WATEULE KUTOJIINGIZA KATIKA MIGOGORO YA KIFEDHA


 Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri, Miji, Manispaa na Majiji 185 hapa nchini wakila kiapo cha maadili ya viongozi leo Ikulu Jijini Dar es salaam.


IKULU JIJINI DAR ES SALAAM,

WAZIRI Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka Wakurugenzi watendaji wateule kuwa makini katika utekelezaji wa majukumu yao ya kazi za kila siku, huku akiwatahadharisha kwamba wasije wakajikuta wanaingia kwenye migogoro ya kifedha na kikazi dhidi ya watendaji wengine pamoja na wananchi wanaoenda kuwaongoza.

Hayo yalisemwa na Waziri Mkuu Majaliwa alipokuwa akizungumza na leo na Wakurugenzi watendaji wateule 185 wa majiji, manispaa, miji na halmashauri za wilaya na kuwataka pia huko waendako waende wakafanye kazi kwenye maeneo yao mapya waliyopangiwa kwa kuzingatia uadilifu, uwajibikaji na uaminifu.

Waziri Mkuu ametoa wito huo leo, kabla hawajatoa viapo vya maadili katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam.

“Jukumu mlilopewa na Mheshimiwa Rais ni nyeti na linahitaji utulivu wa kujituma kwa kila mmoja wenu, mnatakiwa mkafanye kazi kwa uadilifu mkubwa kwa kila mmoja wenu kuwajibika ipasavyo”, alisema Majaliwa.


Majaliwa aliongeza kuwa wao ndiyo injini ya maendeleo katika halmashauri zote hapa nchini katika kusimamia fedha za miradi ya maendeleo ya wananchi, hivyo wanapaswa kuhakikisha wanasimamia fedha za ndani na fedha zinazotoka serikali kuu, juu ya matumizi yake kwa lengo la kupata value for money.

“Mkifika huko ninawasihi mshirikiane na wadau wengine ambao ni wakuu wa mikoa, wilaya, kamati za ulinzi na usalama, wakuu wa idara, watumishi wa idara mbalimbali zilizopo chini yenu na watendaji wa kata na vijiji ili tuweze kufikia malengo yetu tuliyojiwekea ya kuwaletea maendeleo wananchi”, alisisitiza.

Pia aliwaagiza kwa kuwataka wasome taarifa mbalimbali ili waelewe majukumu na mipaka yao ya kazi, maeneo ya utawala  na wajipange kikamilifu katika kusimamia na kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwani imebeba ahadi zilizotolewa na Rais aliyekuwa madarakani sasa, pamoja na Makamu wake wa Rais wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka jana.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan aliwataka wateule hao watambue pia dhamana waliyopewa kuwa viongozi wa halmashauri na kwamba wanakwenda huko kuwa watumishi wa umma na siyo watawala. 

“Wewe ni kiongozi hivyo unapaswa kutengeneza watu wako ili wakusaidie kutekeleza kile ulichotumwa kufanya, fanyeni kazi kwa bidii hivi sasa Tanzania yetu inaenda kwa spidi kali lakini pia mjihadhari na kashfa za matumizi mabaya ya fedha. Msisahau kuwa fedha ni fedheha, ukiitumia vibaya utapata fedheha”, alisema.

Vilevile akiwahutubia wateule hao, Rais Dkt. John Magufuli aliwataka huko waendako wakawe watatuzi wa kero za wananchi badala ya kuwatengenezea migogoro isiyokuwa ya lazima na kuleta kero na matatizo yatakayoweza kufarakanisha jamii, na kurudisha nyuma maendeleo ya wananchi.

“Kaondoeni kero kwa wananchi wa hali ya chini, wako huko wanatozwa kodi ndogo ndogo hata za kuuza mchicha, mtu akivuna mpunga wa kula nyumbani kwake pia anatozwa kodi ni lazima kodi hizi mkazuie kwa sababu tuliahidi kupunguza kero kwa wananchi na siyo kuongeza kero kwao,” alisisitiza.

Alisema ana imani nao kwamba wataenda kutekeleza ilani ya CCM na akawataka waandae mipango yao ya maendeleo kila mmoja kulingana na eneo analolitawala kwa kuitekeleza na sio vinginevyo.

Alisema katika mpango wa maendeleo wa miaka mitano, Serikali imedhamiria kujenga Tanzania yenye uchumi wa viwanda na kuwataka wasimamie kilimo ili mazao yatakayozalishwa yaweze kusindikwa hapa nchini.

No comments: