Sunday, July 24, 2016

HALMASHAURI YA MBINGA YATOA SHUKRANI KWA WADAU WA MAENDELEO



Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

HALMASHAURI ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, imetoa shukrani kwa Wadau wa maendeleo wilayani humo, kwa kutoa msaada wa magari ambayo yametumika kubebea madawati kutoka mjini Songea mkoani humo kwenda wilayani hapa, kwa ajili ya kukalia wanafunzi darasani.

Wilaya hiyo imepata mgawo wa madawati 537 ambayo yametengenezwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Mlale mkoani hapa, kupitia fedha za mfuko wa jimbo ambazo hutolewa na serikali kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo ya wananchi.

Emmanuel Kapinga ambaye ni Ofisa utumishi wa wilaya ya Mbinga, alitoa shukrani hizo kwa niaba ya Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo Gumbo Samanditu, wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake juu ya mkakati wa kumaliza tatizo la madawati kama ilivyoagizwa na Rais Dkt. John Magufuli.


“Upatikanaji wa madawati haya tumeweza kumaliza kabisa tatizo la upungufu lililopo hapa wilayani kwetu, tunawashukuru wadau hawa wa maendeleo hapa Mbinga kwa kutoa magari yao kwenda Songea kuchukua madawati haya ambayo yametengenezwa na JKT kwa ajili ya kusaidia watoto wetu waweze kuandika mwandiko mzuri wanapokuwa darasani”, alisema.

Kapinga alifafanua kuwa katika mkoa wa Ruvuma, halmashauri yake imekuwa ya kwanza kuitika wito huo wa kwenda kuchukua madawati hayo licha ya halmashauri zote mkoani humo, kupewa taarifa husika ya kwenda kuyachukua.

Hata hivyo aliongeza kuwa ufanisi huo umetokana na ushirikiano mzuri uliopo kati ya uongozi wa halmashauri hiyo na wadau hao, hivyo amewapongeza na kuwaomba waendeleze mahusiano hayo mazuri waliyonayo sasa ili kuweza kuendelea kusukuma mbele gurudumu la maendeleo la wilaya hiyo kwa manufaa ya wanambinga na taifa kwa ujumla.

No comments: