Sunday, July 24, 2016

WATOTO WENYE ULEMAVU WA NGOZI MBINGA WAPATIWA MSAADA WA MAFUTA MAALUM YA KUPAKA

Katibu tawala wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Gilbert Simya na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya mji wa Mbinga, Robert Mageni waliosimama nyuma wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wanachama wa chama cha albino wilaya ya Mbinga, baada ya kukabidhi msaada wa mafuta yenye thamani ya shilingi laki 870,000 yaliyotolewa na chama cha walemavu wilayani humo kwa ufadhili wa hospitali ya KCMC ya mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.
Katibu tawala wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Mhandisi Gilbert Simya akikabidhi mafuta maalum ya kuzuia magonjwa ya ngozi kwa watu wenye ulemavu wa ngozi jana, wakati wa kukabidhi msaada wa mafuta hayo yenye thamani ya shilingi 870,000 yaliyotolewa na Chama cha walemavu wilayani humo.


Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

JAMII imetakiwa kuwalea, kuwatunza na kuwajali watu wenye ulemavu wa ngozi albino kwa kuhakikisha kwamba wanaishi katika mazingira mazuri, yenye usalama na sio kuwanyanyapaa pale wanapohitaji mahitaji yao ya msingi.

Aidha Chama Cha Walemavu Tanzania (CHAWATA) tawi la Mbinga mkoa wa Ruvuma kimeshauriwa kuendelea kushirikiana na serikali, ili walemavu hao pia waweze kupata elimu juu ya afya ya usalama wa ngozi pamoja na kutatua matatizo mbalimbali yanayowakabili katika maisha yao.

Hayo yalisemwa na Katibu tawala wa wilaya ya Mbinga, Mhandisi Gilbert Simya wakati alipokuwa akipokea msaada wa mafuta maalum ya kupaka watu wenye ulemavu wa ngozi albino katika hafla fupi iliyohudhuriwa na walemavu hao ambayo ilifanyika kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo uliopo mjini hapa.

Mafuta hayo yalitolewa na Chama hicho cha walemavu kwa watu 87 wenye ulemavu wa ngozi Halmashauri ya mji wa Mbinga, baada ya kuyapokea kutoka kitengo cha magonjwa ya ngozi Hospitali ya KCMC Moshi mkoani Kilimanjaro ambayo yanathamani ya shilingi 870,000.


“Nampongeza Mwenyekiti wa CHAWATA ndugu Martin Mbawala kwa jitihada zake alizozifanya juu ya namna ya kupata mafuta haya, kama chama endeleeni kuwa wabunifu namna ya kulisaidia kundi hili tete la walemavu kwa kuwalea na kuwatunza katika mazingira mazuri”, alisisitiza Mhandisi Simya. 

Vilevile Simya aliongeza kwa kuwataka viongozi wa chama hicho kutumia fursa waliyopewa na wanachama wao, kuhakikisha kwamba wana ainisha matatizo waliyonayo walemavu wa Mbinga na kuyafikisha katika ofisi za serikali ili yaweze kufanyiwa kazi.

Awali akitoa maelezo mafupi juu ya changamoto zinazowakabili albino katika Halmashauri ya mji huo, Mwenyekiti wao Gelioni Nchimbi ambaye ni wa Chama cha maalbino alisema kuwa wanashindwa kuwafikia wanachama wake kwa urahisi kutokana na kukosa usafiri na rasilimali fedha, kwa ajili ya kuwatimizia mahitaji yao ya msingi. 

Nchimbi alifafanua kuwa kukosekana kwa fedha kunakwamisha utendaji kazi na uendeshaji wa shughuli husika, hivyo wanaiomba serikali kuwaangalia kwa jicho la huruma kwa kutatua kero zinazowakabili ili kundi hilo tete liweze kusonga mbele kimaendeleo.

No comments: