Tuesday, July 12, 2016

TUNDURU WAITAKA SERIKALI KUDHIBITI VIKUNDI VINAVYOVURUGA AMANI



Na Steven Augustino,      
Tunduru.

SERIKALI wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, imewataka viongozi wanaounda vikundi ambavyo vimekuwa vikitishia amani katika wilaya hiyo na kuvuruga dini ya kiislam kuacha mara moja tabia hiyo, vinginevyo watachukuliwa hatua za kisheria dhidi yao.

Aidha imewakumbusha kutekeleza majukumu yao kwa kufuata maelekezo yaliyopo katika katiba inayosimamia utekelezaji wa majukumu ya dini yao, chini ya mwamvuli wa baraza linalosimamia maudhui ya dini hiyo (BAKWATA).

Mkuu wa wilaya ya Tunduru Juma Homera alisema hayo juzi, wakati alipokuwa akimwakilisha Mkuu wa mkoa  wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge kwenye sherehe za baraza la Idi  Elfitry zilizofanyika kimkoa wilayani hapa.


Homera alisema kuwa serikali inazo taarifa juu ya uwepo wa vikundi hivyo, pamoja na kazi wanazozifanya na kwamba ili kufikia ufumbuzi imepanga kufanya mazungumzo na viongozi wake, ili kuwaonya wasiendelee na tabia hiyo.

Awali akisoma risala katika maadhimisho hayo, Sheikh Omary Machundo alimweleza Mkuu wa wilaya Homera kuwa, miongoni mwa changamoto zinazotishia kuvuruga amani na dini ya uislamu wilayani humo ni uwepo wa vikundi hivyo visivyojulikana.

Alisema kuwa viongozi wa vikundi hivyo wamekuwa na tabia ya kuandika nyaraka mbalimbali, zenye kuyaruhusu baadhi ya makundi kutoka mataifa ya nje nchi kuingia katika wilaya za mkoa wa Ruvuma, wakisingizia kueneza dini jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa nchi.

No comments: