Thursday, July 7, 2016

MIILI YA WATU WAWILI WALIOKUFA MAJI MTO RUVUMA YAPATIKANA



Na Kassian Nyandindi,
Songea.

MIILI ya watu wawili wanaohofiwa kufa maji katika mto Ruvuma, baada ya boti walilokuwa wakisafiria, imekutwa ikielea kando kando ya mto huo katika kijiji cha Mitomoni wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma.

Kamanda wa Polisi mkoani humo, Zubery Mwombeji ameitaja miili ya watu hao kuwa ni Fadhil Hamis (9) ambaye ni mwanafunzi wa darasa la pili, shule ya msingi Mitomoni na Omary Jela (11) ambaye naye ni wa darasa la tatu katika shule hiyo.

Alifafanua kuwa miili hiyo imepatikana juzi kwa nyakati tofauti ambapo mwili wa kwanza wa Fadhil Hamis ulipatikana majira ya saa 12 asubuhi, ukiwa unaelea juu ya maji jirani na kingo hizo za mto Ruvuma ambapo mwili wa pili wa Omary Jela ulikutwa ukiwa juu ya maji kwenye eneo la kijiji cha Mitomoni, majira ya saa 2 asubuhi.


Alisema kuwa miili hiyo imepatikana kufuatia juhudi za kuitafuta zilizofanywa na wananchi wa vijiji vya Nakawale wilayani Songea na Mitomoni wilayani Nyasa ambapo tangu Julai 2 mwaka huu, ilipotokea ajali hiyo ya boti kuzama na kusababisha watu tisa kufa maji.

Kamanda Mwombeji alisema kuwa mto Ruvuma ambao una mamba wengi pia unakina kirefu na kwamba, juhudi zinaendelea za kuitafuta miili mingine ambayo mpaka sasa haijapatikana.

Vilevile amewaomba wananchi wa vijiji ambavyo vipo kando kando ya mto huo waone umuhimu wa kuendelea kujenga ushirikiano na wenzao wa vijiji vya Nakawale Songea, pamoja na Mitomoni wilayani Nyasa kuitafuta miili ya watu saba ambayo bado haijapatikana.

No comments: