Sunday, July 31, 2016

HALMASHAURI WILAYA YA MBINGA YAJIWEKEA MIKAKATI UPIMAJI WA ARDHI MIJI MIDOGO




Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya  ya Mbinga mkoani Ruvuma, Ambrose Mtarazaki kushoto na baadhi ya Madiwani wa halmashauri hiyo wakimsikiliza kwa makini, Mthamini wa ardhi wa wilaya hiyo, Gabriel Kameka (hayupo pichani) wakati wa mafunzo ya siku moja ya kuwajengea uwezo madiwani hao juu ya umuhimu wa upangaji na upimaji ardhi katika miji midogo ya wilaya hiyo.

Na Kassian Nyandindi,        
Mbinga.

HALMASHAURI ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, imejiwekea mikakati ya kuhakikisha kwamba miji midogo iliyopo katika halmashauri hiyo ardhi yake inapimwa kisheria na kuwafanya wakazi waliopo katika maeneo husika, wasiweze kujenga kiholela.

Aidha katika vijiji kupitia kamati zake, watashirikishwa juu ya mamlaka ya taratibu husika za upangaji wa matumizi ya ardhi na kwamba upimaji huo utashirikisha pia wananchi kwa kuchangia gharama ndogo.

Hayo yalisemwa juzi na Mthamini wa ardhi wilaya ya Mbinga, Gabriel Kameka alipokuwa akitoa mafunzo elekezi ya siku moja kwa Madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo, yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Umati uliopo mjini hapa.

Kameka alifafanua kuwa kwa kutambua hilo serikali iliandaa sera ya ardhi mwaka 1995 pamoja na sheria zake, kwa madhumuni ya kuongoza ugawaji juu ya matumizi bora ya ardhi na kulinda haki zote zilizopo ndani yake.


Alisema kuwa malengo ya semina hiyo ni kuwawezesha madiwani huko waendako katika kata zao, wakaelimisha jamii na kuwezesha viongozi wengine wa umma waweze kutambua juu ya faida za upangaji, upimaji na umilikishwaji wa ardhi ndani ya miji midogo na vijiji.

“Viongozi wa umma mnapaswa katika hili kwenda kuhamasisha wananchi na kuwezesha utafutaji, upatikanaji na utekelezaji wa sheria ya ardhi ili jamii iweze kunufaika kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye”, alisema Kameka.

Alifafanua kuwa lengo kuu la Wizara ya ardhi nyumba na maendeleo ya makazi, ipo kwenye mpango wa kupima kila kipande cha ardhi na kukimilikisha mpaka hapo ifikapo mwaka 2025.

Mthamini huyo wa ardhi wilaya ya Mbinga, Kameka alieleza kuwa kwa kuzingatia hilo halmashauri hiyo inataka iwe ya kwanza kutekeleza agizo hilo kwa kupima kila kipande cha ardhi, kilichopo katika miji midogo na vijiji vyote ndani ya wilaya hiyo.

Pamoja na mambo mengine aliongeza kuwa katika kutekeleza zoezi hilo, itamlazimu kila mmiliki wa ardhi kijijini kulipia gharama za upimaji wa kipande chake cha ardhi  ambapo timu ya wataalamu wa halmashauri hiyo imependekeza kupunguza gharama hizo, ambazo hapo awali ilikuwa ni shilingi 300,000 za upimaji ardhi kwa ekari moja na kufikia shilingi 120,000 kutokana na kipato cha wananchi wake.

Kwa upande wao Madiwani wa halmashauri hiyo, walipongeza juhudi hizo zinazofanywa na wataalamu wake huku wakiunga mkono na kueleza kwamba watakwenda kuelimisha wananchi katika maeneo yao, ili zoezi hilo litakapoanza kutekelezwa liweze kuwa na ufanisi mkubwa.

No comments: