Sunday, July 31, 2016

BASI LA MAKEO LAPINDUKA NA KUUA WATU WATATU DEREVA ASHIKILIWA NA POLISI


Na Kassian Nyandindi,          
Songea.

JESHI la Polisi mkoani Ruvuma, linamshikilia Frank Ndunguru (33) ambaye ni dereva wa Kampuni ya mabasi ya Makeo inayosafirisha abiria kutoka Manispaa ya Songea kwenda wilaya ya Mbinga mkoani humo, baada ya kusababisha ajali ya gari alilokuwa akiendesha kupinduka na kuua watu watatu.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Zubery Mwombeji alisema kuwa tukio hilo lilitokea Julai 30 mwaka huu majira ya saa 1:30 usiku katika kijiji cha Mkako kata ya Mkako wilayani Mbinga, ambapo dereva huyo alikuwa akiendesha gari lenye namba za usajili T. 534 CPV aina ya Mitsubish Rosa, ambalo linamilikiwa na Mohamed Makeo mkazi wa Songea mjini.
Zubery Mwombeji.

Mwombeji alifafanua kuwa chanzo cha ajali hiyo kinatokana na uzembe wa dereva huyo, baada ya kuendesha gari katika mwendo kasi na hatimaye kushindwa kukata kona kali kisha kupinduka mara tatu, baada ya gari hilo kupoteza mwelekeo.

“Dereva wa gari hili yupo mikononi mwa Polisi, tunaendelea kumuhoji na kukamilisha hatua za upelelezi ili aweze kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufikishwa Mahakamani”, alisema Mwombeji.

Kamanda huyo wa Polisi alitoa wito kwa madereva wa magari hapa mkoani Ruvuma, kuzingatia sheria za usalama barabarani, ili isiweze kutokea uzembe kama huo ambao unasababisha watu kupoteza maisha na wengine kuwa na ulemavu wa kudumu.


Alisema kuwa Jeshi hilo litaendelea kuchukua hatua kali kwa madereva wa aina hiyo, ikiwemo kufutiwa leseni zao ili madhara ysiweze kutokea mara kwa mara na kupoteza nguvu kazi ya taifa hili.

“Tunaendelea kuwaelimisha hawa wadau wetu wanaosafirisha abiria kuwa makini barabarani pale wanapoendesha vyombo vya moto, uzembe huu haukubaliki kabisa”, alisema.

Kadhalika aliwataja waliofariki dunia kuwa ni Robert Roter (67) ambaye ni raia wa nchi ya Ujerumani, Cosmas Kambona (54) ambaye ni tingo wa gari hilo mkazi wa Songea mjini na mmoja anakadiriwa kuwa na umri wa miaka 33 ambaye jina lake bado halijatambuliwa.

Aliongeza kuwa katika gari hilo kulikuwa na majeruhi 14 ambapo kati ya hao baadhi yao, walilazwa hospitali ya wilaya Mbinga wameruhusiwa na kwamba 10 bado wanauguza majeraha waliyonayo hospitali ya mkoa Songea.

Pamoja na mambo mengine, Kaimu mganga mfawidhi wa hospitali ya mkoa Songea, Jonas Lulandala amethibitisha kupokea majeruhi hao ambao hali zao bado ni mbaya na vifo hivyo kutokea.

No comments: