Monday, July 4, 2016

SOUWASA WASIKITISHWA NA IDARA YA UJENZI MANISPAA SONGEA KUHARIBU MIUNDOMBINU YAKE YA MAJI



Na Kassian Nyandindi,
Songea.

KAIMU Mkurugenzi wa Mamlaka ya maji safi na Usafi wa Mazingira Manispaa ya Songea (SOUWASA) mkoani Ruvuma, Mhandisi John Kapinga amesikitishwa na idara ya ujenzi katika Manispaa hiyo kuharibu miundombinu ya bomba la maji katika eneo la Stendi kuu ya mabasi ya abiria, ambalo hupeleka huduma hiyo muhimu kwa wakazi wa mtaa wa Mfaranyaki mjini hapa.

Leonidas Gama, Mbunge wa Songea mjini.
Uharibifu huo umefanyika kufuatia msingi uliochimbwa katika eneo la bomba kuu la kupeleka maji katika mtaa huo kwa lengo la kujenga uzio, katika eneo hilo la stendi ili watu wasiweze kuingia hovyo na Manispaa kuweza kukusanya mapato yake.

Masikitiko hayo ya Mkurugenzi huyo wa SOUWASA yalitolewa mbele ya waandishi wa habari, ambao walikwenda Ofisini kwake kwa lengo la kutaka kujua kwa nini ukuta huo unaojengwa katika eneo hilo la stendi ujengwe juu ya bomba hilo ambalo endapo litaharibika wakati wowote ule, Mamlaka hiyo baadaye itakapohitaji kulifanyia marekebisho itashindwa kutokana na kujengwa kwa uzio huo kwa kutumia tofari za saruji.


Kapinga alisema taratibu za ujenzi huo hawajashirikishwa na kwamba haiwezekani bomba hilo la maji lijengwe kwa ajili ya kuhudumia jamii halafu juu yake, ujengwe ukuta huo bila wao kujua na kutoa ushauri namna ya kutekeleza jambo hilo.

“Manispaa yetu kuna mapungufu makubwa ya ushirikishwaji, jambo hili mnalotuambia ndio kwanza tunalisikia kutoka kwenu ninachojua haya yote yanatokana na ushirikishwaji kutoka kwa hawa wenzetu viongozi wa Manispaa hii kuwa mdogo, lakini wangeweza kutushirikisha tungewapatia ushauri mzuri nini wakifanye”, alisema Kapinga.

Akifafanua juu ya wananchi kulalamikia kuharibiwa kwa bomba hilo alisema kuwa watafuatilia suala hilo, kuweza kuona ni namna gani linatengenezwa haraka ili kuweza kurejesha huduma husika kwa wananchi na kuweza kuondokana na adha wanayoipata sasa ya kukosekana kwa huduma ya maji.

Kaimu Mkurugenzi huyo wa Mamlaka ya maji safi na Usafi wa Mazingira katika Manispaa ya Songea, aliongeza kuwa anashangazwa na ujenzi wa uzio huo katika eneo hilo la stendi kuu kwani unawafanya kuharibu mipango yao ya ujenzi wa tenki kubwa la maji hapo baadaye, ambalo inabidi lijengwe kwa ajili ya kuendelea kupanua mtandao wa huduma ya maji safi kwa wananchi.

“Katika eneo hilo pia tunatarajia kujenga tenki kubwa la maji sasa leo hii wanapojenga uzio huu tutapita wapi, vitu kama hivi walipotaka kuvifanya walipaswa kutushirikisha”, alisema.

Pamoja na mambo mengine alipoulizwa Mhandisi wa ujenzi wa Manispaa ya Songea, Godfrey Majuto alisema kuwa changamoto za mabomba ya maji huwa wanakutana nazo mara nyingi pale wanapotaka kufanya shughuli za ujenzi wa miundombinu husika katika Manispaa hiyo.

Majuto alieleza kuwa anaushangaa uongozi wa Mamlaka hiyo ya maji safi na Usafi wa Mazingira katika Manispaa ya Songea, kusema kwamba jambo hilo hawakushirikishwa wakati taratibu za ujenzi wa uzio wa stendi hiyo zinafanyika.

No comments: