Saturday, July 2, 2016

MWANASHERIA WA TAKUKURU MAKETE NJOMBE ANASWA KWA RUSHWA


Na Mwandishi wetu,
Njombe.

MWANASHERIA wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilaya ya Makete mkoani Njombe na mlinzi wa Ofisi za taasisi hiyo wilayani humo, wanashikiliwa na Takukuru wakituhumiwa kwa pamoja kuomba na kupokea rushwa.

Watumishi hao wanatuhumiwa kuomba rushwa ya shilingi 600,000 kutoka kwa mtumishi anayetuhumiwa kughushi vyeti, vilivyomuwezesha kupata ajira.

Kamanda wa TAKUKURU mkoani hapa, Charles Nakembetwa alimtaja Mwanasheria huyo kuwa ni Frednand Nsakuzi na Julius Hassan ambaye ni mlinzi wa ofisi za taasisi hiyo.


Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Nakembetwa alisema kwamba watumishi hao waliomba rushwa kwa mtumishi huyo ili kuweza kuficha ukweli wa taarifa alizohusishwa nazo.

Kamanda huyo wa taasisi hiyo alisema kuwa ofisi yake kwa kushirikiana na mteja wao huyo, waliweka mtego uliofanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao.

Alisema katika mtego uliotegwa Juni 28 mwaka huu, watuhumiwa hao walipokea shilingi 100,000 kama malipo ya awali katika tukio lililofanyika kati ya saa moja na mbili usiku.

“Walikamatwa wakati wakipokea kiasi hicho cha fedha, kinyume na kifungu cha 15 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007”, alisema.

Hata hivyo alisema kuwa uchunguzi unaendelea kufanyika na kwamba watuhumiwa hao watafikishwa Mahakamani wakati wowote kuanzia sasa, ili waweze kujibu tuhuma hiyo inayowakabili.

No comments: