Monday, August 1, 2016

MAZITO: MBINGA KUSAMBAZA MASHINE ZA KUKUSANYIA MAPATO KATIKA VIJIJI VYOTE




Mweka hazina wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Joseph Mazito akiwaonesha madiwani (hawapo pichani) mashine  mojawapo ya kisasa ya kukusanyia mapato aina ya Portable Printer, ambazo zimenunuliwa na halmashauri hiyo kwa ajili ya kusambaza katika vituo na taasisi za serikali kwa lengo la kudhibiti mapato. (Picha na Muhidin Amri)
Na Kassian Nyandindi,        
Mbinga.

KATIKA kuhakikisha kwamba agizo la serikali la kuboresha ukusanyaji wa mapato yake linatekelezwa ipasavyo, halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma imejiwekea mikakati ya kununua na kusambaza mashine za Kieletroniki (EFD’S) katika vijiji vyote vilivyopo wilayani humo.

Aidha hadi kufikia mwezi Julai mwaka huu, imeweza kununua mashine hizo 20 zenye thamani ya shilingi milioni 17 na kuanza kuzisambaza katika maeneo husika ambako tayari zimeanza kufanya kazi iliyolengwa.

Taarifa hiyo ilitolewa na Mweka hazina wa halmashauri ya wilaya Mbinga, Joseph Mazito alipokuwa akiwasilisha mada husika kwa Madiwani wa halmashauri hiyo katika mafunzo elekezi ya ukusanyaji mapato ndani ya wilaya hiyo.


Mazito alifafanua kuwa mpango wa halmashauri yake ni kupeleka mashine hizo katika vijiji vyote 118 vilivyopo wilayani humo na kwamba mpaka sasa watendaji husika, wanaofanya kazi ya kukusanya mapato wamekwisha pewa mafunzo juu ya namna ya kutumia mashine hizo.

“Waheshimiwa Madiwani, tunaomba mtambue kwamba mtu ambaye atakuwa mbali na suala hili la ukusanyaji mapato mjue kwamba huyo hatufai katika kufikia lengo la maendeleo ya wilaya yetu, tumchukulie hatua”, alisisitiza Mazito.

Aliongeza kuwa mategemeo ya halmashauri ya Mbinga, hadi kufikia mwezi Desemba mwaka huu watakuwa wamepeleka mashine zote za kukusanyia mapato kwenye kila kijiji, huku akiwataka Madiwani hao kujenga ushirikiano na wataalamu wake ndani ya wilaya ili kuweza kufikia malengo hayo waliyojiwekea.

Mweka hazina huyo alisisitiza kwamba, kwa mtu yeyote atakayebainika anakwepa kulipa ushuru atachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufikishwa Mahakamani na kutozwa faini kulingana na kosa alilofanya, hivyo amewataka watendaji husika waliopewa dhamana ya kusimamia suala hilo kuwa makini katika utendaji wa kazi zao.

Kufuatia uwepo wa mikakati hiyo kwa upande wao, Madiwani hao walisema hawatakubali kuona uzembe unafanyika katika utekelezaji wa zoezi hilo hivyo wapotayari kuhakikisha kwamba, wanakuwa bega kwa bega ili mapato yao yaweze kukusanywa kikamilifu na kwenda kutekeleza miradi ya maendeleo ya wananchi katika maeneo husika wilayani humo.

No comments: