Tuesday, August 16, 2016

LONGA WAKULIMA WALALAMIKIA KUIBIWA KAHAWA YAO



Na Kassian Nyandindi,         
Mbinga.

WANANCHI wa kijiji cha Longa kata ya Mkumbi wilaya ya Mbinga mkoa wa Ruvuma, wamelalamikia kitendo cha wizi wa kahawa zaidi ya magunia 100 ambao umefanyika kijijini humo na watu wasiojulikana.

Hali hiyo imeelezwa kwamba, kahawa iliyoibwa ni ile ambayo ilianikwa kwenye vichanja nje ya ghala la kuhifadhia kahawa tayari kwa kusafirishwa kwenda Kiwanda cha kukoboa kahawa Mbinga (MCCCO) kilichopo mjini hapa.

Kufuatia tukio hilo walinzi wawili ambao walikuwa wakilinda katika eneo la ghala la kuhifadhia kahawa hiyo, wanashikiliwa na mgambo katika mahabusu ya kata hiyo wakidaiwa kuiba kahawa ambayo ilianikwa kwenye vichanja hivyo.


Wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti wananchi hao ambao ni wakulima wa zao hilo, walisema kahawa yao imeibwa katika mazingira ya kutatanisha majira ya usiku Agosti 11 mwaka huu.

Mwenyekiti wa chama cha ushirika Longa, Angelus Kimonile aliwataja walinzi ambao wanawashikilia kuwa ni Jacob Komba na Anton Ndimbo wakiwataka waeleze bayana juu ya wizi huo, uliofanyika kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria za kuwafikisha mahakamani.

“Hawa walinzi tumewashikilia kwa lengo la kuwahoji na tunawataka watueleze mpaka wizi huu unafanyika wao walikuwa wapi, tunamashaka nao huenda wao ndio waliocheza mchezo huu mchafu”, alisema Kimonile.

Pia aliongeza kuwa tukio hilo linahusishwa na mgogoro uliodumu kwa muda mrefu kwa baadhi ya wanachama wa ushirika huo, kuwakataa viongozi waliopo madarakani wakiwataka waondoke na uchaguzi ufanyike upya kuwachagua wengine.

Alisema kuwa mgogoro huo umedumu kwa miaka miaka miwili ambapo wanachama wanataka uundwe uongozi mpya, kutokana na uliopo sasa kutokuwa na imani nao jambo ambalo halijatekelezwa hadi sasa.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Gombo Samandito aliwaambia waandishi wa habari kwamba kufuatia tukio hilo ameunda timu ya kufuatilia suala hilo, ili liweze kufikishwa kwenye vyombo vya kisheria.

No comments: