Wednesday, August 10, 2016

LUMEME NYASA WALIA NA NAIBU WAZIRI WA ELIMU TEKINOLOJIA NA MAFUNZO YA UFUNDI WAMTAKA KUTEKELEZA AHADI ZAKE



Na Kassian Nyandindi,            
Nyasa.

WANANCHI wanaoishi katika kijiji cha Lumeme kata ya Lumeme wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma wamemtaka Naibu Waziri wa Elimu Tekinolojia na Mafunzo ya Ufundi, Injinia Stella Manyanya kutatua kero mbalimbali za wananchi wake katika sekta ya elimu wilayani humo, ili waweze kusonga mbele kimaendeleo.

Injinia Stella Manyanya.
Aidha Waziri huyo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Nyasa, walisema hivi karibuni alitoa ahadi ya vifaa vya kiwandani kwa ajili ya ujenzi wa choo cha matundu manne kwa wanafunzi shule ya msingi Mbanga, iliyopo katika kata hiyo lakini ni muda mrefu umepita hakuna utekelezaji alioufanya mpaka sasa.

Walifafanua kuwa choo kilichopo sasa katika shule hiyo kimebomoka na kwamba wanafunzi wanapata shida pale wanapohitaji kujisaidia, ambapo hulazimika kutumia vyoo vya walimu au wakati mwingine huenda kujisaidia katika pori lililokuwa karibu na shule hiyo.


Hayo yalisemwa kwa nyakati tofauti na wananchi hao kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini humo, wakati walipokuwa wakiweka mikakati yao ya kusimamia na kuchangia shughuli za maendeleo za kijiji cha Lumeme.

Walisema kuwa wanamshangaa Mbunge wao tokea alipotoa ahadi ya vifaa hivyo vya kiwandani kwa ajili ya ujenzi wa choo hicho, hakuna utekelezaji alioufanya na kwamba pale anapopigiwa simu, ili waweze kumweleza kero zao simu yake imekuwa ikiita kwa muda mrefu bila kupokelewa.

Mwenyekiti wa kijiji cha Lumeme Michael Ndunguru alisema kuwa hali hiyo inawakatisha tamaa kwani wao walikwisha andaa tofari, mchanga na mafundi watakaoweza kufanya kazi ya ujenzi wa choo hicho lakini walichokuwa wakisubiri ni vifaa hivyo vya kiwandani ambavyo Mbunge wao aliahidi kuwapatia ili waweze kutatua kero hiyo kwa kukamilisha ujenzi wake.

Pia mwandishi wa habari hizi alipomtafuta kwa njia ya simu Injinia Manyanya ili aweze kutolea ufafanuzi juu ya malalamiko hayo ya wananchi wake, simu yake ilikuwa ikiita kwa muda mrefu bila kupokelewa. 

Kufuatia hali hiyo, Ndunguru alimpongeza Kamanda wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilayani Nyasa, Cassian Njowoka ambapo kamanda huyo baada ya kupewa taarifa juu ya tatizo hilo aliweza kutoa vifaa hivyo kwa ajili ya ujenzi wa choo cha wanafunzi hao wa shule ya msingi Lumeme, vyenye thamani ya shilingi milioni 1.8.

“Ndugu zangu wananchi msaada huu tulioupata leo hii, tunapaswa sasa kuchukua hatua ya haraka kuanza mara moja ujenzi wa choo hiki ili watoto wetu wasiendelee kupata taabu kama mnavyoona hapa tumepewa mifuko ya saruji, bati, nondo na marumaru za kuweza kutandika chini ya sakafu”, alisema Ndunguru.

Pamoja na mambo mengine Mwenyekiti huyo wa kijiji cha Lumeme, alimtaka Njowoka kuendelea kuwa na moyo wa kuendelea kusaidia wananchi wa wilaya hiyo, ili waweze kuondokana na kero mbalimbali zinazowakabili katika kukuza sekta ya elimu.

No comments: