Sunday, August 14, 2016

WAUGUZI MBINGA WATISHIA KUISHITAKI MAHAKAMANI KURUGENZI SACCOS

Upande wa kulia ni Mbunge wa Jimbo la Mbinga mjini mkoani Ruvuma, Sixtus Mapunda akipeana mkono kwa lengo la kuagana na mganga mkuu wa hospitali ya halmashauri ya mji wa Mbinga, Elisha Robert mara baada ya kumaliza kuzungumza na wauguzi wa hospitali hiyo.


Na Kassian Nyandindi,          
Mbinga.

WAUGUZI wa idara ya afya, hospitali ya Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma wameulalamikia uongozi wa Chama cha akiba na mikopo, Kurugenzi SACCOS kilichopo mjini hapa kwa kushindwa kuwalipa madai yao ya fedha kwa miaka mingi huku wakieleza kuwa, watakwenda kuushtaki uongozi husika Mahakamani ili waweze kupata fedha zao.

Aidha walisema kuwa madai wanayodai ni yale ambayo yanatokana na makato mbalimbali wanayokatwa katika mishahara yao, hivyo hawaoni sababu ya kuendelea kuwa wanachama katika SACCOS hiyo kutokana na manyanyaso wanayoyapata.

Hayo yalisemwa na Wauguzi hao walipokuwa wakizungumza na Mbunge wa Jimbo la Mbinga mjini, Sixtus Mapunda katika kikao maalum kilichoketi jana katika jengo la hospitali hiyo mjini hapa.


Walisema kuwa licha ya suala hilo kufikishwa katika ngazi mbalimbali ya ofisi za serikali, utekelezaji wake umekuwa hauzai matunda na kwamba walimuomba Mbunge huyo aingilie kati ili waweze kupata haki zao za msingi.

Kwa upande wake Mbunge Mapunda alipokuwa akitolea ufafanuzi juu ya malalamiko hayo, alisema kuwa atalifanyia kazi kwa kushirikiana na mamlaka husika ili Wauguzi hao waweze kulipwa madai yao.

Hata hivyo Mapunda aliwashauri watumishi hao wa idara ya afya waweke utaratibu wa kuanzisha chama chao cha akiba na mikopo, ili waweze kuondokana na usumbufu kama huo wanaoupata sasa.

No comments: