Tuesday, August 16, 2016

NJOWOKA ATOA MSAADA WA TAIRI NNE ZA GARI KWA KITUO KIKUU CHA POLISI NYASA

Kutoka upande wa kulia ni Mkuu wa Polisi wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, Shaban Mpwaga akipokea msaada wa tairi nne za gari la kituo kikuu cha Polisi wilayani humo kutoka kwa Kamanda wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wa wilaya hiyo, Cassian Njowoka.

Kutoka kushoto Mkuu wa Polisi wilaya ya Nyasa, Shaban Mpwaga akipokea msaada wa mashine ya Printer kutoka kwa Kamanda wa Umoja wa Vijana Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilayani humo, Cassian Njowoka. Mashine hiyo ilipokelewa kwa ajili ya matumizi ya kituo kikuu cha Polisi wilaya ya Nyasa. (Picha zote na Gwiji la Matukio Ruvuma)
Na Kassian Nyandindi,        

Nyasa.

MKUU wa Polisi wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, Shaban Mpwaga amemshukuru na kumpongeza Kamanda wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wa wilaya hiyo, Cassian Njowoka kwa kutoa msaada wa tairi nne za gari la kituo kikuu cha Polisi wilayani humo zenye thamani ya shilingi milioni 4.4.

Aidha alisema kuwa gari la kituo hicho ambalo tairi zake zimekuwa kipara, wakati mwingine askari wake wanashindwa kutekeleza majukumu yao kikazi kutokana na tairi zilizopo kwisha muda wake wa matumizi.

Shukrani hizo zilitolewa jana na Mkuu huyo wa Polisi wilaya ya Nyasa kwenye hafla fupi ya makabidhiano ya msaada huo, iliyofanyika katika viwanja vya kata ya Kingirikiti wilayani hapa.

Mpwaga alifafanua kuwa licha ya kupewa msaada huo pia Njowoka siku za nyuma aliwahi kuwapatia msaada wa kompyuta, printa mbili za kisasa na karatasi rimu katoni mbili kwa ajili ya kuweza kusaidia kufanyia kazi za Polisi kama vile kuchapa barua za aina mbalimbali.


Kwa upande wake Kamanda wa UVCCM wilayani humo, Njowoka alisema kuwa kutokana na mahusiano ya chama na serikali kuwa mazuri hivyo aliona kuna kila sababu kutoa msaada huo, ili uweze kusaidia jamii katika kutekeleza majukumu ya kimaendeleo.

Njowoka alieleza kuwa hata wananchi wengine ambao ni wazawa wa wilaya hiyo ambao wanaishi nje ya Nyasa, wanapaswa kuwa na moyo wa kwenda kusaidia wananchi kwa kutoa michango ya kimaendeleo ili wilaya iweze kupiga hatua mbele za maendeleo kwa haraka.

“Sisi tuliozaliwa katika wilaya hii na waalika wananyasa wenzangu wote popote pale walipo, wakumbuke kuja kuwekeza na kutoa michango itakayotufanya tupige hatua mbele na kukuza uchumi wetu”, alisema.

No comments: