Saturday, August 20, 2016

NJOWOKA: WANACCM TUACHE KUTENGENEZA MAJUNGU

Kamanda wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, Cassian Njowoka akikabidhi msaada wa mashine ya Fotokopi kwa Mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo, Francis Homanga ambapo mashine hiyo aliikabidhi kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya chama hicho wilayani humo.

Cassian Njowoka akikabidhi msaada wa Kompyuta kwa Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Nyasa, Francis Homanga kwa ajili ya matumizi ya chama hicho wilayani humo.


Na Kassian Nyandindi,       
Nyasa.

VIONGOZI na Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, wametakiwa kuacha kutengeneza majungu na mifarakano ndani ya chama hicho na kwamba endapo wataendekeza mambo hayo, huenda wakasababisha malumbano na kukigawa chama.

Cassian Njowoka.
Aidha viongozi wa CCM wameshauriwa kutembelea wananchi wao katika maeneo yao mara kwa mara, ili kukifanya chama kiweze kuwa endelevu katika kupigania haki na maendeleo husika katika jamii.

Hayo yalisemwa na Cassian Njowoka ambaye ni Kamanda wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilayani Nyasa, alipokuwa akizungumza na wananchi wa kata ya Kingirikiti wilayani humo katika hafla fupi ya kukabidhi msaada wa vifaa vya chama hicho.


Njowoka alikabidhi msaada wa mashine ya kisasa ya fotokopi, printa, kompyuta mbili pamoja na katoni mbili za rimu za karatasi kwa ajili ya kuchapia barua za aina mbalimbali.

Alisema kuwa vifaa hivyo vitaweza pia kukisaidia chama hicho, kuanzisha mradi wake utakaosaidia kujipatia fedha za kuendeshea chama na kuepukana na mtindo wa kuwa omba omba.

Pamoja na mambo mengine Kamanda huyo wa UVCCM ameweza kulifanyia matengenezo gari la Chama cha mapinduzi wilayani humo, ambalo liliharibika kwa muda mrefu lilikuwa halifanyi kazi, matengenezo ambayo yamegharimu fedha za kitanzania shilingi milioni 2.3.

Vilevile kwa upande wake akipokea msaada huo, Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Nyasa Francis Homanga alisema kuwa wanamshukuru kwa mwenendo wake mzuri wa kukisaidia chama mara kwa mara, huku akimtaka moyo huo alionao aendelee nao kwa manufaa ya kuisaidia jamii.

“Nampongeza Njowoka kwa jitihada hizi anazozifanya kwa uzalendo wake wa kuchangia maendeleo ya wilaya hii, mambo mengi ya kimaendeleo pale tunapomuomba msaada amekuwa mwepesi kutusaidia”, alisema Homanga.

Homanga alibainisha kuwa Njowoka ameweza kuchangia mifuko ya saruji katika ujenzi wa zahanati, miundombinu ya maji, shule za msingi na sekondari pamoja na ufungaji wa mfumo wa umeme jua katika maeneo ya kutolea huduma za afya vijijini.

No comments: