Sunday, August 28, 2016

RC RUVUMA ASEMA HALI YA USAFI SONGEA SIO YA KURIDHISHA

Na Kassian Nyandindi,          
Songea.

MKUU wa mkoa wa Ruvuma Dkt. Binilith Mahenge amesema kuwa hali ya usafi katika Manispaa ya Songea mkoani humo, sio ya kuridhisha hivyo ameutaka uongozi husika wa Manispaa hiyo kuchukua hatua za haraka kunusuru hali hiyo ili isiweze kuleta madhara, ikiwemo magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu.

Mji wa Songea.
Dkt. Mahenge amemtaka Mkurugenzi mtendaji Tina Sekambo na Meya wake wa Manispaa hiyo Alhaj Abdul Mshaweji, kutumia sheria ndogo ndogo za mazingira ambazo zitaweza kusimamia suala hilo na kuufanya mji huo kuwa safi.

Dkt. Mahenge alisema hayo juzi kwenye kikao kilichohusisha watumishi wa serikali, taasisi za umma, madiwani, wafanyabiashara na wazee ambacho kilifanyika mjini hapa.

Alisema kuwa utunzaji wa mazingira na masuala ya usafi ni jambo la lazima ambalo kila mwananchi, anapaswa kulitekeleza ili kuweza kuzuia magonjwa ya mlipuko yanayoweza kujitokeza na kuleta madhara katika jamii.


“Kampeni ya usafi katika mji wetu wa Songea ni jambo la lazima kwa kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi, agizo langu kwa Manispaa ondoeni taka zote zilizopo kwenye maghuba’’, alisisitiza Dkt. Mahenge.

Mkuu huyo wa mkoa alieleza kuwa jukumu la kufanya usafi wa mazingira ni endelevu na kwamba halmashauri zinapaswa kusimamia hilo kwa kuhakikisha taka zote mkoani humo, zinakusanywa toka majumbani kwa wananchi na kupelekwa sehemu maalumu kwa ajili ya kuziteketeza ili zisiweze kuleta madhara.

Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa Manispaa ya Songea, Sekambo alitoa agizo kwa idara ya afya katika Manispaa hiyo kuhakikisha kwamba wanashirikiana kwa pamoja katika kutekeleza jambo hilo, ili kuweza kufikia malengo husika ya ukusanyaji wa taka zote zilizopo katika mji huo.

Sekambo alisema kuwa maeneo ya katikati ya mji wa Songea yanaridhisha kwa usafi, isipokuwa katika maeneo ya pembezoni mwa mji huo ndiyo ambayo yamekuwa machafu na watu wamekuwa wakitupa taka hovyo, ambapo alitoa rai kwamba kwa atakayekamatwa atachukuliwa hatua za kisheria.


“Naagiza juhudi za kufanya usafi ziongezwe ili Manispaa yetu iweze kuwa katika hali ya usafi, taasisi za shule na wafanyabiashara tushirikiane pia kutekeleza jambo hili la usafi wa mazingira”, alisema Sekambo.

No comments: