Wednesday, August 10, 2016

WANANCHI MBINGA WATISHIA KUANDAMANA KWENDA OFISI YA MKUU WA WILAYA WAKITAKA SERIKALI IWASAIDIE KUNUSURU JENGO LAO

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge.


Na Kassian Nyandindi,         
Mbinga.

WANANCHI wa kijiji cha Ilela kata ya Mikalanga wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma wamesema kwamba ipo siku wataandamana kuelekea ofisi ya Mkuu wa wilaya hiyo, kwa lengo la kuiomba serikali kuingilia kati mgogoro ambao umedumu kwa muda mrefu sasa kati yao na taasisi ya Ansary Muslim Youth Center, iliyopo mjini hapa ambayo inadaiwa kupora jengo lao la biashara.

Jengo hilo ambalo ni maarufu kwa jina la Ilela, ni kitega uchumi ambacho kilijengwa na wananchi hao mwaka 1980 kwa lengo la kupangisha wafanyabiashara wa aina mbalimbali, ili waweze kujipatia fedha kwa ajili ya kufanyia maendeleo yao.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa kijiji hicho Anton Komba alisema kuwa mgogoro huo umekuwa ukiwakera kutokana na kudumu kwa zaidi ya miaka 15 na hakuna mafanikio, hivyo wanaiomba serikali iwasaidie ili waweze kunusuru jengo lao.


Komba alisema kuwa licha ya suala hilo kufikishwa kwa viongozi wa ngazi ya wilaya hakuna mafanikio yanayoonesha kuzaa matunda juu ya tatizo hilo.

Alisema kuwa taasisi ya Muslim Youth Center imejiuzia jengo hilo kwa shilingi milioni 5 kupitia aliyekuwa mpangaji ambaye anafahamika kwa jina la Yordan Konzo bila kufuata taratibu husika.

Kadhalika alibainisha kuwa Konzo alifanya tukio hilo la kupiga mnada jengo hilo na kuliuza kwa fedha hizo, akidai kwamba uongozi wa kijiji cha Ilela alikuwa anaudai shilingi 900,000 jambo ambalo sio la kweli.

“Wamiliki wa jengo hili ni wananchi wenyewe na hata tukifanya leo hii uthaminishaji wa jengo hili mali zilizopo pale ni zaidi ya milioni 800, inakuwaje yeye apige mnada na kuliuza kwa shilingi milioni tano?”, alihoji Komba.

Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa suala hilo ambalo lipo pia mezani kwa viongozi wa wilaya ya Mbinga, utekelezaji wake umekuwa ukisuasua hivyo wanajipanga kwenda kumuona Mkuu wa wilaya hiyo ili jengo lao libakie mikononi mwa wananchi.

Vilevile mwandishi wa habari hizi alipofanya mahojiano na Yordan Konzo ili aweze kutolea ufafanuzi juu ya jambo hilo, alisema yeye alifuata taratibu husika wakati anapiga mnada jengo hilo ili aweze kupata fedha zake anazokidai kijiji hicho.

Hata hivyo Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye alisema kwamba jambo hilo atalifanyia kazi ili kuweza kumaliza mgogoro huo usiweze kuendelea na mali za wananchi hao, zibakie katika mikono yao kama ilivyokuwa hapo awali.

No comments: