Monday, August 1, 2016

SIMBACHAWENE AWATAKA WATUMISHI WAZEMBE WAPISHE ILI NAFASI ZAO ZA KAZI ZICHUKULIWE NA WENGINE



Waziri wa TAMISEMI George Simbachawene akisalimiana na watumishi halmashauri ya wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, alipokuwa katika ziara yake ya kikazi hivi karibuni.
Na Yeremias Ngerangera,      

Songea.

WAZIRI wa nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) George Simbachawene, amewataka watumishi wa umma ambao hawaendani na kasi ya utendaji kazi wa serikali hii ya awamu ya tano, kwa hiari yao wapishe ili nafasi hizo zichukuliwe na watu wengine.

Hayo yalisemwa na Waziri huyo wakati alipokuwa akizungumza hivi karibuni na wakurugenzi na wakuu wa idara wa halmashauri za mkoa wa Ruvuma, kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea mjini hapa.

Aidha Simbachawene alikemea watumishi hao akisema hakuna sababu ya wao kuandamana kwa lengo la kudai haki zao, ikiwemo suala la kupandishwa madaraja kwani hivi sasa mtumishi atapandishwa daraja kutokana na elimu yake aliyonayo na uwezo wake wa utendaji kazi kiutumishi.


Simbachawene alifafanua kuwa mtumishi atakayeonekana kutotekeleza vizuri majukumu yake, hatapandishwa cheo au daraja badala yake ataendelea kubaki kama alivyo mpaka pale atakapofikia hatua ya kustaafu.

Pamoja na kutoa msimamo huo, Waziri huyo alipokea taarifa za maendeleo kwa kila halmashauri iliyopo mkoani hapa ambapo pamoja na mambo mengine aliwataka wakurugenzi, wakuu wa wilaya pamoja na wenyeviti wa halmashauri kuweka mikakati ya kuhakikisha kwamba uchumi wa halmashauri zao unakuwa kwa kasi ili wananchi waweze kuondokana na umaskini.

Awali akisoma taarifa ya maendeleo ya mkoa huo Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge alisema kuwa mkoa wake una halmashauri nane ambazo ni Mbinga mji, Mbinga vijijini, Tunduru, Nyasa, Madaba, Songea vijijini, Songea Manispaa na halmashauri ya wilaya ya Namtumbo.

No comments: