Friday, August 5, 2016

HOJA YA STENDI YAWAFANYA MADIWANI SONGEA WAVUTANE WANANCHI WAZOMEA KIKAONI

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge.

Na Kassian Nyandindi,
Songea.

MVUTANO mkali umetokea katika kikao cha baraza la Madiwani Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, kufuatia baadhi ya madiwani kupinga hoja inayohusu kutumika kwa stendi ya zamani iliyopo mjini hapa kwa mabasi yanayosafirisha abiria kwenda nje ya mkoa huo, wakitaka mabasi hayo yaanze safari zake katika kituo kipya cha Msamala kilichopo mbali na mji huo.

Kufuatia hali hiyo lilibuka kundi la Wananchi ambao nao walihudhuria kusikiliza mkutano huo na kuanza ghafla kuzomea madiwani waliokuwa wakipinga hoja hiyo, jambo ambalo lilihatarisha kuvunjika kwa amani ndani ya kikao hicho kilichoketi juzi kwenye ukumbi wa Manispaa hiyo mjini hapa.

Aidha katika baraza hilo Meya wa Manispaa hiyo Abdul Mshaweji, Mbunge wa Songea mjini, Leonidas Gama na madiwani wengi waliokuwa wakiunga mkono hoja hiyo walionekana kushangiliwa na wananchi hao huku wengine wakipaza sauti zao wakisema, wanataka mabasi hayo ya abiria yaanze safari zake katika stendi hiyo ya zamani na sio vinginevyo.

Wananchi hao walisikika wakieleza kuwa wamekuwa wakipata shida kwa muda mrefu kwenda kupanda mabasi katika stendi hiyo ya Msamala ambayo ipo mbali na mji huo, jambo ambalo hulazimika kutumia fedha nyingi kukodi taxi mpaka kufika huko Msamala.


Baada ya kuonekana hali inazidi kuwa mbaya ndipo Mkuu wa wilaya ya Songea Palolet Mgema, alichukua jukumu la kuingilia kati kunusuru hali hiyo ili machafuko yasiweze kutokea baada ya kuonekana dalili kwamba kuna baadhi ya kikundi cha madiwani ndani ya kikao hicho kutaka kuanza kuleta fujo.

“Ninaona mnataka kukiharibu kikao kwa hoja ambayo haina nguvu, kama kuna agenda muhimu mnataka ijadiliwe fuateni kanuni na taratibu za kuwasilisha hoja siyo kila mtu anasimama na kuzungumza bila utaratibu, mimi nikiwa Mkuu wa wilaya sipo tayari kuona uvunjifu wa amani ukitokea sitamvumilia mtu yeyote wala kikundi chochote humu ndani, ambacho kitasababisha uvunjifu wa amani”, alisema Mgema.

Mkuu huyo wa wilaya, Mgema alisema iwapo kama diwani anahoja muhimu binafsi ya kupinga suala hilo alipaswa kufuata utaratibu na kuiwasilisha agenda hiyo mapema, kabla ya kikao hicho kuanza na sio kukurupuka na kuanza kupinga wakati tayari lilikwisha pitishwa katika maamuzi husika.

Hali ya utulivu iliporejea Diwani wa kata ya Msamala kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Issack Lutengano, alipinga hoja ya mabasi kuanza kupakia abiria stendi hiyo ya zamani huku akisema kwa jazba kwamba Meya wa Manispaa hiyo, Mshaweji aache kuendesha baraza kwa kuendeshwa na wapambe wachache.

Kauli hiyo ya Lutengano ilianza kuzua mvutano mkali kati yake na Meya huyo ambaye licha ya kujitahidi kumwelekeza afuate kanuni za vikao, hata hivyo hakutaka kumsikiliza badala yake alikuwa akiendelea kuongea kwa jazba huku wananchi waliofika kusikiliza kikao hicho, wakianza kuwazomea tena madiwani hao ambao walikuwa wakipinga hoja ya mabasi ya kusafirisha abiria mjini hapa kuanza safari zake eneo la stendi hiyo ya zamani.

Naye Diwani wa kata ya Ruvuma, kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Rashid Mososa alisema yeye haoni dhambi mabasi hayo kuanza safari zake katika stendi ya zamani hadi stendi mpya ya Msamala na kwamba aliwataka Madiwani wenzake kuwaonea huruma wananchi, ambao wanatoka mbali hulazimika kutumia usafiri wa taxi kwa kukodi kwa gharama kubwa kwenda kupanda mabasi katika stendi hiyo mpya ambayo ipo mbali na mji wa Songea.

Kwa upande wake naye Naibu Meya, Consolatha Kilowoko wa CCM aliwataka madiwani wenzake kuwa na ubinadamu na kuacha kuwaumiza wananchi kwa kuendekeza maslahi yao binafsi, badala ya kutetea wananchi wenye maisha magumu.

Hata hivyo Mbunge wa viti maalum wa Chama Cha Mapinduzi Judith Mbogoro aliwataka madiwani hao kuunga mkono hoja ya mabasi kuanzia stendi hiyo ya zamani, ili kuweza kuwasaidia hata wanawake wajawazito na watoto wadogo waweze kupata huduma ya usafiri kwa ukaribu zaidi hoja ambayo baadaye iliungwa mkono na wengi wao katika kikao hicho cha baraza la madiwani.

No comments: