Thursday, August 4, 2016

TASAF TUNDURU YAENDELEA NA UHAKIKI WA MAJINA YA WANUFAIKA WAKE



Na Steven Augustino,
Tunduru.

MFUKO wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF) wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, unaendelea na zoezi lake la uhakiki wa kupitia taarifa za wanufaika wake ikiwa ni jitihada ya kuweza kubaini kama kunawanufaika ambao hawajakidhi vigezo husika na hatimaye waweze kuondolewa.

Juma Homera, Mkuu wa wilaya Tunduru.
Hali hiyo imetokana na uwepo wa taarifa kwamba kuna baadhi ya watoto ambao wamekwisha maliza shule, lakini bado wanaendelea kupokea fedha za ruzuku kutoka katika mfuko huo.

Mshauri wa TASAF wilaya ya Tunduru, Christian Amani alisema hayo wakati alipokuwa akizungumza na wanufaika wa vijiji vya Mkasale na Liwanga vilivyopo tarafa ya Namasakata wilayani hapa.

Amani alisema kuwa tayari mfuko huo, umekwisha sambaza fomu maalum za kufanya uhakiki huo kwa walimu wa shule zote za msingi na sekondari zenye wanafunzi wanaonufaika na mpango huo ili kuweza kubaini, tatizo hilo lipo wapi na hatimaye kulitafutia upembuzi yakinifu.

“Walimu wanaoshirikiana na wazazi kuficha taarifa za kumaliza shule watoto wao hawana tofauti na wafanyakazi hewa, hivyo ni lazima hatua zichukuliwe haraka ili kuweza kuwaondoa katika mfumo wetu wa utoaji ruzuku kwa kaya maskini”, alisema.


Alisema katika zoezi hilo, TASAF haitamuonea mtu bali itatekeleza majukumu yake kwa kuwapunguzia pato lao kulingana na idadi ya watoto waliokuwa wakinufaika na mpango huo.

Naye Mratibu wa Mfuko huo wa maendeleo ya jamii wilaya ya Tunduru, Stanley Haulle alisema kuwa katika utekelezaji wa zoezi hilo mkuu wa kaya ambaye atabainika kuwa na watoto hewa wanaopokea ruzuku, atapunguziwa pato lake kwa wastani wa shilingi 2,000 kwa kila mwezi hivyo kwa kaya iliyokuwa na watoto wanne nayo itapunguziwa shilingi 16,000.

Aliongeza kuwa katika utekelezaji wa zoezi hilo, awali waliweza kuondoa kaya maskini 484 zisizokuwa na sifa baada ya kujiridhisha hawakukidhi vigezo husika.

No comments: