Tuesday, August 16, 2016

EPZA YALALAMIKIWA KUTOWALIPA FIDIA WANANCHI MWENGEMSHINDO SONGEA

Rais Dkt. John Magufuli.


Na Julius Konala,           
Songea.

BAADHI ya wananchi wa kata ya Mwengemshindo Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma ambao maeneo yao yametwaliwa na shirika la EPZA kwa kipindi cha miaka tisa iliyopita bila kuwalipa fidia yoyote, wamemuomba Waziri wa viwanda na biashara, Charles Mwijage kuingilia kati suala hilo ili waweze kupata haki yao ya msingi.

Ombi hilo lilitolewa juzi na wananchi hao mbele ya Mbunge wa jimbo la Songea mjini Leonidas Gama, katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa michezo wa kata hiyo na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa siasa na serikali.

Walisema kuwa tangu maeneo yao yachukuliwe wamekuwa wakiishi katika maisha magumu kutokana na kuzuiwa kuendesha shughuli yoyote ile, ikiwemo kilimo cha mazao ya chakula na biashara ili waweze kujipatia kipato katika maisha yao ya kila siku.


Akizungumza katika mkutano huo mmoja kati ya wakazi wa eneo hilo, Otmary Komba alisema kuwa kutokana na kucheleweshwa kulipwa fidia ya maeneo yao baadhi yao, wanashindwa hata kusomesha watoto wao shule huku familia zikikosa pia mahali pa kuishi.

Kwa upande wake Mbunge huyo aliwataka wananchi hao kuwa watulivu wakati serikali inaendelea kushughulikia suala hilo, na akaongeza kwamba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limekwisha pitisha bajeti kwa ajili ya fidia ya maeneo yao.

Gama alisema kuwa eneo hilo lenye ukubwa usiopungua ekari 5,000 litakuwa pekee kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda mbalimbali, hivyo amewataka wazazi kusomesha vijana wao ili waweze kunufaika na ajira pindi viwanda hivyo vitakapoanza kufanya kazi.

“Ndugu zangu sitaweza kuzungumzia kwa kina juu ya suala la baadhi ya wananchi ambao maeneo yao yamechukuliwa na EPZA kwa kuwa shauri hilo lipo Mahakamani linashughulikiwa kisheria, siruhusiwi kulizungumzia hapa mpaka mchakato wake utakapokuwa umekwisha”, alisema Gama.

No comments: