Thursday, August 25, 2016

DC MBINGA ASISITIZA UJENZI WA VYOO SHULE ZA MSINGI NA SEKONDARI

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, Robert Mageni akizungumza juzi katika kikao cha baraza la madiwani wa mji huo kilichofanyika kwenye ukumbi wa jumba la maendeleo mjini hapa, katikati ni Mwenyekiti wa halmashuri hiyo Kipwele Ndunguru na wa mwisho kushoto ni Makamu wake Mwenyekiti Tasilo Ndunguru.
Na Kassian Nyandindi,          
Mbinga.

MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Cosmas Nshenye amewataka watendaji waliopo katika halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani humo kuhakikisha kwamba wanatekeleza kwa haraka zoezi la ujenzi wa vyoo bora mashuleni, ili wanafunzi waweze kuepukana na magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu.

Zoezi hilo la ujenzi wa vyoo hivyo alisema kuwa anataka lianze mara moja kuanzia sasa, kwa shule za msingi na sekondari ambazo kuna tatizo la upungufu wa vyoo ili kuweza kuepukana na watoto kujisaidia vichakani.

Agizo hilo la Mkuu huyo wa wilaya lilitolewa juzi kwenye kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya mji huo, kilichofanyika mjini hapa katika ukumbi wa Jumba la maendeleo.


“Suala la ujenzi wa vyoo ni lazima litekelezwe kuanzia sasa, nataka mikakati ya kuhakikisha kwamba kila shule ya msingi na sekondari inatekeleza jambo hili mapema na kwa kasi kubwa”, alisisitiza Nshenye.

Alibainisha kuwa yeye hapendi kusikia wataalamu katika wilaya hiyo wanavutana bali anatarajia kusikia wanapigania maendeleo ya wananchi kwa faida ya kizazi cha sasa baadaye.

Nshenye alisema kuwa kama wataishia kulumbana maana yake hawataweza kufikia malengo husika ya kuhudumia wananchi, hivyo amewataka wafanye kazi kwa kujituma na sio muda mwingi kukaa maofisini.


“Ndugu zangu mtumishi yeyote aliyeajiriwa na serikali asitafute utajiri kwenye makaratasi, nikisema hivi najua mnanielewa yatupasa tukubali kwamba ulikubali kuajiriwa kwa ajili ya kuwatumikia wananchi”, alisema.

No comments: